Mpango wa kuvipatia umeme visiwa vyote unatia moyo

MOJA kati ya maeneo ambayo serikali imepata mafanikio makubwa ni usambazaji wa umeme vijijini. Hivi sasa, hata asiye na macho anaona hatua iliyofikiwa, ambapo kila mahali ukienda, ama utakuwa umeme unawaka; au utakuta kuna miundombinu ya nishati hiyo inawekwa.

Kelele zilizokuwa zikisikika kila mara katika maeneo mengi nchini, za kudai nishati hizo, kwa hakika zimepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hivi karibuni Rais John Magufuli alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuongeza kasi katika kusambaza umeme kwa kuwaunganishia Watanzania wengi zaidi nishati hiyo.

Pia, alilitaka shirika hilo kuachana na umeme unaozalishwa kwa kutumia majenereta; na kutilia mkazo umeme unaozalishwa kwa njia ya gesi na maji. Kwamba umeme wa gesi na maji huzalishwa kwa gharama nafuu, ukilinganisha na ule unaozalishwa kwa kutumia majenereta. Tunaunga mkono hatua hiyo ya serikali ya kuhimiza usambazaji umeme nchini.

Kwa mujibu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuna vijiji 7, 800 nchi nzima havijafikiwa na umeme. Lakini, jambo la kutia moyo ni kuwa Waziri Muhongo anasema serikali itahakikisha vijiji vyote hivyo, vinapata umeme mwaka huu.

Aidha, tunaipongeza serikali kwa kutangaza kuwa visiwa vyote vya bahari na maziwa, yakiwemo Victoria, Tanganyika na Nyasa, vitafikiwa na umeme. Akizindua Bodi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) mwishoni mwa wiki, Profesa Muhongo alieleza kwamba serikali itafikisha umeme sehemu za mbali na gridi, ikiwemo visiwa vyote vya bahari na maziwa. Kwamba visiwa vyote ndani ya miaka miwili au mitatu, lazima vitapata umeme.

Kwamba serikali haipitishi ‘cable’ chini ya bahari au chini ya ziwa, bali itatumia umeme wa nguvu za jua. Kazi hiyo itafanywa na kampuni binafsi ambazo zote ni za Watanzania. Ni wazi serikali imefanya kazi nzuri katika kipindi kifupi tu.

Mathalani, mwaka 2008 wakati REA inaanza kazi, wakazi wa vijijini Tanzania Bara waliokuwa na fursa ya kutumia umeme, walikuwa chini ya asilimia kumi tu ya watu wote. Lakini, hadi kufikia Desemba 30 mwaka jana, idadi ya wenye fursa ya kutumia umeme vijijini iliongezeka hadi kufikia asilimia 49.5. Ni dhahiri hii ni hatua kubwa na inatia moyo.