Muungano ni silaha dhidi ya maadui zetu

WATANZANIA kama kawaida yao, jana walionesha mshikamano wao wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni kwa kusherehekea maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tena kwa mara ya kwanza katika makao makuu ya nchi yetu mjini Dodoma.

Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, marais wastaafu na viongozi wengine waandamizi wa serikali, wabunge na wananchi kwa ujumla wao, walishikamana kwa kuonesha utulivu wa hali ya juu katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, kulikofanyiwa maadhimisho hayo yaliyopambwa kwa gwaride na maonesho ya vyombo vya ulinzi na usalama, ngoma na nyimbo kutoka Bara na Visiwani.

Hakuna ubishi kwamba Watanzania wana kila sababu ya kufurahi na kuonesha mshikamano wao kutokana na ukweli kwamba miaka 53 katika umri wa jambo lolote lile si haba, ukizingatia kwamba kulikuwa na changamoto mbalimbali zilizoukabili muungano huo, lakini zilishughulikiwa ipasavyo.

Kati ya kero 15 zilizokuwa zinaukabili muungano huo, kero 12 zilipatiwa ufumbuzi na kubakiwa na kero tatu, ambazo pia kwa mila na desturi za watanzania, zinashughulikiwa kwa amani na utulivu na kwa utaratibu muafaka.

Rais Magufuli bila kumung’unya maneno wakati akizungumza jana katika maadhimisho hayo, alisema muungano ndiyo silaha yetu, muungano ndiyo jembe letu na muungano ndiyo ushindi wetu na kwamba utalindwa kwa nguvu zote.

Alisisitiza kwamba, “Kamwe asijitokeze mtu wa kuuvunja muungano kwani atavunjika yeye.’’ Jukumu la kuulinda na kuimarisha muungano, Rais ameliweka wazi kwamba ni la kila mtanzania, tena kwa kuchapa kazi.

Manufaa na faida za muungano wetu, sote ni mashahidi na kwamba atakayekwenda kinyume na matakwa yetu, basi hatua na taratibu zichukuliwe dhidi yake, badala ya kusubiri kufikia hatua ya kuturudhisha nyuma ya hapo tulipokwishafikia.

Hapa tungependa kusisitiza pia kwamba amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, ndiyo dira yao na kwamba aliye nje ya mshikamano huo, asipewe nafasi ya kutuvuruga.

Muungano huu ulioanzishwa na waasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume miaka 53 iliyopita, tutaendelea kuuenzi kwa vizazi vyetu vilivyopo sasa na vijavyo.

Wahenga walisema ‘Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu’. Sisi tayari tumekwisha kuwa wamoja na hatuna mpango wa kutengana, kwani huo siyo utamaduni wa Watanzania. Mungu Ibariki Tanzania.