Kuanzishwe chombo kuratibu kueneza Kiswahili kimataifa

HAKUNA ubishi kwamba lugha ya Kiswahili inazidi kushika kasi ndani na nje ya bara la Afrika kutokana na ukweli kwamba inazungumzwa, inasomeka na inafundishika tofauti na lugha nyingine barani Afrika ambazo ni vigumu kuwa na vipengele vyote kama ilivyo kwa lugha ya Kiswahili.

Mizizi na uwezo wa lugha hiyo kuendelea kuenea kwa kasi kunatokana na ukweli kwamba viongozi wetu kwa kuanzia na Baba wa Taifa hili la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya mwanzo kabisa ya kupigania Uhuru wetu kutoka katika mikono ya ukoloni wa Mwingereza, alitumia lugha hiyo kuwasiliana na Watanzania kwa kuwahamasisha wapinge ukoloni hadi kufikia hatua ya kupata Uhuru wetu Desemba 9, mwaka 1961 tena bila kumwaga damu.

Lakini pia ndiyo lugha ya Taifa na ambayo tunayoitumia kuanzia watoto wetu wanapokua tangu utotoni na kuingia katika msafara wa elimu kwa kuanza kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Hakuna mtanzania wa kweli ambaye hajui lugha ya Kiswahili licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120.

Vyombo vya habari ni nyenzo nyingine kubwa inayotumika katika kueneza lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Vyombo hivyo vya habari ni pamoja na magazeti, redio na televisheni ambavyo tuna haki ya kutembea kifua mbele kwa kujidai kwamba hakuna chombo cha habari katika hivyo nilivyovitaja ambavyo nje ya lugha ya Kiingereza, kinatumia lugha za kikabilia katika uendeshaji wake.

Kupitia vyombo hivyo nguvu ya lugha ya Kiswahili inazidi kuongezeka na kujichimbia tofauti na nchi nyingine za Afrika ambazo baadhi ya vyombo vyao vya habari hutumia lugha za makabila na hivyo kupunguza kwa kiasi fulani mshikamano na umoja wa kitaifa.

Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli imetoa umuhimu wa pekee katika matumizi ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili kwa shughuli za kitaifa na kimataifa, ikiwa ni msukumo mwingine wa kuhakikisha kwamba lugha hiyo inazidi kupaa katika nyanda za kitaifa na kimataifa.

Tunapenda kutoa pongezi maalumu kwa Rais wetu kwa maamuzi yake ya makusudi ya kukuza lugha yetu lakini pia kwa kuonesha njia ya kutaka kuwapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili kwenda kufundisha majirani zetu wa Rwanda ambao tayari wameshatoa maamuzi ya kutumia Kiswahli kufundishia katika shule zao.

Kuna fursa ambayo ipo wazi na inasubiri kutumiwa na Watanzania kujinasua kwa makusudi na changamoto ya ukosefu wa ajira, ni pamoja na fursa hiyo ya kufundisha lugha ya Kiswahili usoni mwa macho ya kimataifa.

Hakuna ubishi kwamba Tanzania ndiyo nchi ambayo iko katika nafasi nzuri ya kutoa walimu wazuri kwenda kufundisha lugha hiyo popote duniani kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika kutokana na sababu zilielezwa hapo juu na ambazo hakuna nchi nyingine yenye kubarakiwa kwa fursa hizo.