Ni aibu timu ya Serengeti Boys kukosa udhamini

TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inaendelea na maandalizi yake ya fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Gabon mwezi ujao.

Serengeti Boys ipo Yaounde, Cameroon ambapo wiki ijayo itacheza mechi mbili za kirafiki na vijana wenzao wa Cameroon kabla ya kwenda Libreville, kwa fainali hizo ambazo Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza.

Timu hiyo ilianza maandalizi yake mapema mwezi huu ikiweka kambi Morocco ambapo imecheza mechi mbili dhidi ya Gabon zote ikishinda kwa mabao 2-1. Kwa mwenendo wa timu hiyo inatoa picha kwamba mambo hayatakuwa mabaya Libreville na kwamba vijana wetu wanaweza kututoa kimasomaso na kufika mbali kwenye michuano hiyo.

Serengeti imepangwa kundi B kwenye michuano hiyo ikiwa na Mali, Niger na Angola huku kundi A likiwa na timu za wenyeji, Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana. Timu nne za juu kwenye michuano hiyo zitacheza fainali za kombe la dunia kwa vijana Novemba mwaka huu, India.

Kumekuwa na hamasa ya michango kwa muda mrefu sasa, wadau wa michezo na watanzania kwa ujumla wakihamasishwa kuichangia timu hiyo, hasa kwa vile haina mfadhili, kwa mujibu wa wanakamati hali ya michango si haba.

Lakini tunalojiuliza, hivi ni kweli timu inayowakilisha nchi kwenye michuano mikubwa kama hiyo ikakosa udhamini mpaka sasa? Kampuni zote hizi, wawekezaji wote hawa kweli hakuna hata inayojitokeza kudhamini vijana hao ambao hakuna shaka kwamba mpaka walipofika juhudi zao zinaonekana?

Wakati wa kuisaidia timu hiyo ni sasa, si kusubiri icheze nusu fainali na kwenda kombe la dunia ndipo kampuni zipigane vikumbo kutaka kuidhamini. Kampuni, wafanyabiashara onyesheni uzalendo kwa kuidhamini timu hii, haiingii akilini fursa hiyo inashindwa kutumika, jitokezeni kuidhamini timu ili vijana wapiganie taifa lao wakiwa na uhakika na udhamini mnono. Hili halikubaliki, na ni aibu kwa timu hiyo mpaka sasa kukosa udhamini hata wa maji ya kunywa baada ya mazoezi.