Wenye vyeti feki ni funzo Mei Mosi

LEO Watanzania wanaungana na wenzao duniani, kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi). Hii ni siku inayoadhimishwa kila mwaka kwa wafanyakazi katika sekta mbalimbali kutafakari kazi, mazingira, changamoto na ufanisi katika maeneo ya kazi ili kuongeza ufanisi kwa siku zijazo.

Hii yote inatokana na umuhimu wa mwanadamu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija katika maeneo ya kazi. Katika maadhimisho haya yanayofanyika mwaka huu kitaifa mkoani Kilimanjaro huku mgeni rasmi akiwa Rais John Magufuli, tunawapongeza wafanyakazi wote waliojitoa kwa moyo kufanya kazi kwa uadilifu katika mazingira na maeneo ya kazi huku wakizingatia kuwa haki siku zote huendana na wajibu.

Kwetu sisi maadhimisho ya mwaka huu ya Mei Mosi, yameangukia katika kipindi kinachohitaji tafakuri ya kina ili kurekebisha makosa na “kuzisafisha siku za usoni.” Tunasema hivyo kwani mwishoni mwa wiki Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angella Kairuki, alimkabidhi Rais Magufuli ripoti yenye orodha ya watumishi wa umma 9,932 wenye vyeti feki vya elimu.

Gazeti hili katika toleo la jana, lilichapisha majina yote yaliyopo kwenye ripoti ili umma uwatambue kama alivyosema Rais. Sisi tunampongeza Rais Magufuli na wasaidizi wake kwa nia ya dhati kurudisha heshima ya elimu, hadhi na uadilifu wa watumishi wa umma; kwa kuhakikisha wote wana sifa zinazostahili.

Ni dhahiri wenye vyeti feki wamesambaza sumu ya utendaji duni katika sekta mbalimbali huku wakitumia muda na nguvu nyingi, kupiga kelele na njia nyingine za kuficha udhaifu wao, badala ya kutumikia umma kwa ufanisi.

Sisi tunasema ingawa kwa wakati huu wapo wachache wanaonung’unikia hatua hii, lakini ukweli ni kuwa unaipeleka Tanzania katiia njia sahihi na iliyopaswa kuwapo miaka mingi iliyopita.

Wakati tukitoa pongezi hizo, tunaishauri Serikali kupitia vyombo vinavyohusika, kuhakikisha kosa lililofanyika nyuma la kutoa mwanya watu kuwasilisha nyaraka feki za kidanganyifu na kujipatia ajira, halirudiwi wala kupata nafasi tena.

Funzo lingine ni kuhakikisha anafanya kila jambo kwa njia halali iliyojaa uaminifu na uadilifu ili Tanzania isiwe kichaka la wahuni wanaoishi kwa njia za mkato, bali waadilifu na wanaozingatia kazi kwa juhudi na maarifa huku wakizingatia kuwa haki na wajibu vinategemeana kama kuku na yai.

Ingawa tunajua waliokumbwa na msukosuko huo, wameathirika kwa kiasi kikubwa walioguswa waichukulie, hali hii kama changamoto maishani na kwamba huo, sio mwisho wa maisha yao na wategemezi wao. Hivyo, watafakari upya na kuanza maisha kwa njia nyingine za kiuadilifu na halali ili maisha yaende sawia kwa manufaa ya familia zao na taifa kwa jumla.