Neema sasa imefunguliwa kwa wafanyakazi

JUZI ilikuwa Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi). Kitaifa siku hii iliadhimishwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kitaifa, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.

Maadhimisho hayo yamekuja zikiwa ni siku chache tangu mkuu wa nchi huyo apokee ripoti yenye orodha ya watumishi wa umma 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kughushi kujipatia ajira serikalini.

Katika maadhimisho hayo ya Mei Mosi, Rais akasisitiza kuwa, Serikali haina mzaha katika hili na kwamba itaendelea kuwabaini wote wanaofanya udanganyifu katika umri wao ili wachelewe kustaafu utumishi wa umma, na hata wenye vyeti vya taaluma visivyostahili (vya kughushi).

Katika kuudhihirishia umma wa Watanzania kuwa lengo la Serikali kufanya uhakiki wa vyeti ni zuri kwa manufaa ya Taifa, Rais aliwatangazia Watanzania neema ya ajira 52,000 katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18 unaoanza Julai mosi mwaka huu, baada ya kukamilika zoezi za uhakiki wa vyeti.

Sisi tunasema, tangazo la ajira 52,000 za Watanzania wenye sifa stahiki, ni neema kwa wengi waliokosa ajira eti kwa sababu tu, zimekaliwa na watu “walioziiba au kuzivamia”. Hii si tu ni neema kwao watakaoajiriwa, bali pia wategemezi wao, uchumi na maendeleo ya Tanzania.

Katika hili tunaipongeza Serikali hasa tukikumbuka pia namna ilivyotangaza hadharani kuwa baada ya mambo hayo kukamilika, kutakuwa na ongezeko la mwaka katika mishahara ya wafanyakazi huku katika mwaka huu wa fedha, watumishi wakianza kupandishwa vyeo na madaraja ya kazi.

Ndiyo maana tunasema, kazi imebaki kwa wafanyakazi wenyewe maana neema imefunguliwa kiasi kwamba, hata wafanyakazi waliokuwa wanatumiwa vibaya na waajiri au wakubwa wao kwa manufaa yao waajiri, sasa hawataipata nafasi hiyo.

Kimsingi, tunasema neema imefunguka kwa wafanyakazi Tanzania baada ya mkuu wa nchi kupiga marufuku, mtumishi yeyote kuhamishwa bila kupewa malipo stahiki ya uhamisho huo.

Tunasema neema kwa sababu, watumishi kunyimwa au kucheleweshewa na hatimaye kupoteza haki za malipo ya uhamisho imekuwa kero ya muda mrefu kwa wafanyakazi wengi nchi na imechangia kuwakatisha tamaa wafanyakazi wengi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Rais Magufuli amewatangazia neema nyingine wafanyakazi Tanzania aliposema Serikali ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuanzisha bima ya ajira itakayochukua nafasi ya fao la kujitoa.

Katika kuonesha umakini kutekeleza neema hizi, Rais alisema muswada wa sheria hiyo ya bima ya ajira ukiwasilishwa mezani kwake, atausani siku hiyo hiyo. Kimsingi, neema zinazofunguka sasa ni taswira ya wazi ya nia ya Serikali kuhakikisha ofisi na taasisi za umma, zinakuwa safi kwa sifa za kielimu, kitaaluma, kiutendaji na kiuadilifu.

Ndiyo maana tunasema, kazi sasa imebaki kwa wafanyakazi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa maana, neema imefunguliwa Tanzania.