Serikali iendelee kuondoa kodi zinazokera wakulima

MOJA ya kero kubwa inayokabili wakulima wengi nchini ni utitiri wa kodi mbalimbali katika mazao ya chakula na biashara, kama vile pamba, chai na kahawa. Wakulima wamekuwa wakipaza sauti zao binafsi, kupitia kwa vyama vyao vya ushirika pamoja na viongozi wao, wakiwemo wabunge.

Kutokana na hali hiyo, tumevutiwa na kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bungeni mjini Dodoma wakati wa hotuba yake ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Waziri Mkuu alitangaza kuwa serikali imefuta baadhi ya tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa ambazo ni kero kwa wakulima. Miongoni mwao ni tozo hizo ni kodi ya Sh 450,000 iliyokuwa inatolewa na kila kiwanda cha kuchambua pamba nchini kwa ajili ya kuchangia mbio za Mwenge.

Tozo nyingine iliyofutwa kwa zao la pamba ni ada ya vikao vya halmashauri za wilaya, ambayo ni Sh 250,000. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, katika zao la chai, kodi iliyofutwa ni ya moto na uokoaji ; na kwenye zao la kahawa, tozo iliyoondolewa ni ada ya leseni ya kusindika kahawa ya dola za Marekani 250.

Ni wazi kuwa hatua hizo kubwa alizotangaza, zimekuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu na wakulima nchini ili kuwaondolea kero. Tunaamini kuwa kufutwa kwa tozo hizi, ambazo zilikuwa kero kubwa, ni utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli kwa wakulima nchini.

Hatua hizi zitainua uwezo wa wakulima, ambao umekuwa ukizoroteshwa na tozo hizi zinazowapunguzia kipato na faida. Tuna imani hatua hizi zitachochea kwa namna ya pekee ari ya wakulima katika kuendesha kilimo cha biashara chenye tija. Mamlaka zinazohusika zinatakiwa kuanzia sasa kutafuta njia nyingine za kupata fedha kwa shughuli zao.

Kama shughuli hizo ni za muhimu na inabidi ziendelee, basi kinachotakiwa siyo kupeleka madeni kwa wakulima. Tunaamini kwamba serikali itaendelea kuchambua kwa kina kodi, tozo na ada zilizobaki, ambazo ni kero na zisizokuwa na tija katika sekta nyingine za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwezesha wananchi wa kawaida, kunufaika zaidi na jasho lao.

Kwa ujumla, kauli hiyo iliyotolewa na Waziri Mkuu inaonesha kwamba serikali inajali watu maskini, ikiwemo wakulima wadogo, ambao wamekuwa wakibeba mizigo, ambayo kimsingi inawanyima haki ya kufurahia jasho lao.

Tunaipongeza serikali kwa kusikiliza kilio hiki cha muda mrefu cha wakulima nchini; na ni matumaini yetu kwamba itaendelea kutatua kero zao ili waweze kujituma zaidi na kufaidi matunda ya jasho lao.