Wanahabari ni vema kujiimarisha kitaaluma

MOJA ya habari iliyochapishwa na gazeti hili jana ilibeba kichwa cha habari ‘Dk Mwakyembe: Waandishi zingatieni weledi.’ Kwanza tukumbushane kwamba mtajwa katika habari hiyo ni Dk Harrison Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Dk Mwakwembe alikuwa anazungumza juzi mjini Mwanza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani. Hakuna ubishi kwamba kila taaluma ina maadili na miiko yake ambayo wana taaluma hawana budi kuifuata na kuzingatia katika utendaji wa kazi waowza kila siku ili kutoa huduma inayotarajiwa kwa umakini na uhakika.

Misingi hiyo huwekwa ili kudhibiti wale ambao ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, hujikuta wakitenda kinyume cha taratibu za kazi husika. Hakuna ubishi kwamba, Waziri Mwakyembe, mwenye dhamana na sekta ya habari amekumbusha waandishi wajibu wao ili kuweza kufanya kazi zao kwa uhakika na weledi zaidi.

Kazi kuu za mwandishi wa habari ni pamoja na kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii. Sekta ya habari imepanuka na kuongezeka kutoka zile za kimapokeo ya magazeti, radio na televisheni hadi kwenye mitandao ya kijamii ambayo nayo inatoa habari kwa jamii kwa haraka zaidi kuliko vyombo hivyo vya mapokeo ingawa umuhimu wa vyombo hivyo uko paleplae na unazidi kuongezeka.

Katika hali kama hiyo ya mitandao ya kijamii, waandishi wa habari hawana budi sasa kwenda mbele zaidi kwa kutumia taarifa zinazopatikana moja kwa moja kwenye mitandao kama wazo la habari na hivyo kulifanyia kazi ipasavyo ili kuwafikishia taarifa kamili wanajamii.

Umuhimu huu unatokana zaidi na ukweli kwamba, baadhi ya taarifa kwenye mitandao ya kijamii wakati mwingine hupotosha au kukosa uthibitisho kutoka kwa wahusika ndani ya habari.

Kwa mwanahabari kutekelezaji wajibu wake kwa kuitendea haki taarifa aliyoipata kwa kupata pande zote zinazohusika katika habari, ndiyo kutekeleza weledi ambao ni muhimu katika taaluma yenyewe.

Hapa tungependa kutoa mwito kwa waandishi wa habari wajiendeleze kitaaluma katika, ngazi mbalimbali kwa lengo la kuongeza uwezo siyo katika eneo la habari peke yake bali hata katika taaluma nyingine ikiwa ni pamoja na sheria, uchumi, maendeleo ya jamii, siasa na nyinginezo ili kuwaweka katika hali ya uwanja mpana wa kufanya uchambuzi wa uandishi wa uhakika katika sekta hizo muhimu katika jamii.

Sisi tunatumia maadhimisho na fursa hii kukumbushana kuwa, Tanzania hivi sasa vipo vyuo vya ngazi mbalimbali kuanzia ya vyeti, diploma, digrii na kuendelea juu zaidi. Mwanafunzi kwa sasa halazimiki kusoma akiwa muda wote shuleni, bali anaweza akaendelea na masomo huku akifanya kazi zake pia.

Ni kwa msingi huo tunasema, wanahabari watumie mwanya huu, kujiendeleza kielimu kama ilivyo kwa wanataaluma wengine ili kuimarisha na kuboresha sekta ya habari na uzalishaji wa habari muhimu kwa jamii.