Tuwaombee Serengeti Boys

FAINALI za 12 za Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, zinaanza rasmi kesho Jumapili nchini Gabon na kushirikisha jumla ya timu nane. Serengeti Boys, timu ya taifa ya vijana ya Tanzania ya umri huo, ndio inaiwakilisha nchi katika mashindano hayo, na tayari iko huko.

Timu hiyo iko katika Kundi B pamoja na Angola, Mali na Niger wakati Kundi A linaundwa na wenyeji Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana. Kwa miaka mingi, Tanzania imeshindwa kufuzu kwa fainali hizo za Afrika kwa timu za umri wowote ikiwemo ile ya wakubwa, Taifa Stars, ambayo kwa mara ya mwisho ilicheza fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyikia Lagos, Nigeria.

Ni miaka 37 tangu Tanzania iliposhiriki kwa mara ya kwanza na mwisho katika fainali za Afcon, hivyo wapenzi wa soka wamekuwa na kiu kubwa ya kuona moja ya timu zao za taifa zikishiriki fainali hizo.

Ni matumaini makubwa kwa wadau wa michezo na hasa soka kuwa, Serengeti Boys baada ya kujiandaa kwa muda mrefu ndani na nje ya nchi, wakati umefika kufanya maajabu katika soka la Afrika na dunia.

Timu hiyo endapo itafuzu kucheza nusu fainali, basi moja kwa moja itakuwa imekata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika India Novemba mwaka huu. Serengeti Boys ilianza na kambi ya nchini kabla ya kwenda Morocco ambako ilijichimbia huko kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kumalizia Cameroon, ambako walicheza na wenyeji mchezo wa kujipima nguvu.

Hakuna ubishi kuwa, vijana wetu wamepata mazoezi ya kutosha kabisa na wamejiandaa vya kutosha tayari kwa mashindano hayo makubwa, ambayo yanaweza kuitangaza vizuri nchi endapo timu yetu itafanya vizuri.

Mbali na Serengeti Boys, pongezi zingine kubwa ziende kwa walezi wa timu hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Jamal Malinzi walioiwezesha kupata maandalizi hayo makubwa. Ni matumaini yetu kuwa wachezaji wa timu hiyo watajituma na kucheza kwa bidii ili kuhakikisha wanaitoa kimasomaso Tanzania katika soka hilo la Afrika na baadae dunia.

Pia ni kazi ya Watanzani waliobaki nyumbani kuiombea dua timu yetu hiyo ili iweze kufanya kile ambacho hakijawahi kufanywa kwa zaidi ya miaka 35 na kuweka rekodi kwa kufika mbali zaidi.

Hakuna kisichowezekana katika soka, ila tu baada ya kupata maandalizi ya kutosha kilichobaki ni kuwaombea dua vijana wetu ili waepukane na majeruhi na matatizo mengine, ili waweze kufanya vizuri. Kila mtu kwa imani yake tuwaombee vijana wetu ili waweze kufanya vizuri nchini Gabon na baadae nchini India katika Kombe la Dunia.

Kila la heri Serengeti Boys tuko pamoja nanyi.