Wananchi wana haki ya kujua ukweli wa uendeshaji wa benki

JANA katika gazeti letu tuliandika kuhusu maamuzi ya Benki Kuu ya Tanzania kufunga benki nyingine baada ya kukosa sifa ya kuendelea kuhudumia wananchi. Maamuzi ya kuifunga Mbinga Community Bank Plc, yamefanyika muda mchache baada ya benki nyingine ye FBME kufungwa.

Ingawa benki zote hizo zimefungwa kwa kukosa sifa tofauti za kuendelea kuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi, kufungwa kwao kunaleta maswali mengi kwa wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wakihimizwa kuweka fedha katika benki.

Kusitishwa kwa shughuli za kibenki kwa benki hizo mbili kwa maana ya kufutiwa leseni zake za biashara na moja kuwekwa chini ya mfilisi si dalili njema kwa wenye amana na waliokuwa wakitumaini huduma za benki hizo kwa shughuli mbalimbali za kifedha.

Pamoja na kupongeza Benki kuu kuchukua maamuzi hayo mapema kuokoa fedha za wananchi kwa kiasi kinachowezekana, sisi tunaona ipo haja kwa Benki kuu Kutoa taarifa ya ujumla kuhusu hali ya kifedha katika benki zetuj ili kuondokana na hofu ambayo inaweza kuwakumba watu wa kawaida.

Aidha elimu kuhusu mwenendo wa benki nchini na hadhari zinazostahili kwa wananchi kuhusiana na suala la uwekaji amana nchini inatakiwa kuwekwa katika mazingira ya wazi ili wananchi watambue hasara, faida za benki mbalimbali nchini.

Mbinga Community Bank Plc ambayo sasa imewekwa katika chini ya ufilisi na kuteuliwa kwa Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi kuanzia juzi,kunaonekana kwa nje kama janga hasa kutokana na watu kuhamasishwa na kuendelea kuweka akiba huku wakiwa hawaoni tatizo la ndani.

Ni kazi ngumu sana kwa mwananchi wa kawaida kutambua eneo salama la kuweka fedha zake kwani imani ya kawaida ni kuwa kila aliyepewa leseni anaweza kuhifadhi fedha na kuzifanyiakazi inavyostahili.

Tunaamini kwamba upungufu huu wa mtaji na ukwasi ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha, haukutokea kwa siku moja na hili ndilo ambalo tungelipenda wananchi waelimishwe.

Pamoja na BoT kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha, Benki Kuu ya Tanzania isiishie tu kuwataka wenye amana, wadai na wadaiwa wa benki zote hizo mbili kuwa wavumilivu lakini pia kuanza kutoa elimu kuhusu mienendo ya benki na benki salama maana yake nini.

Tunasema hivyo kwa kuwa mwanzoni mwa wiki BoT ilitangaza kuifilisi na kufungia shughuli zake hapa nchini benki ya FBME na sababu ilikuwa baada ya kushindwa kufanya shughuli za kibenki kutokana na kutuhumiwa na taasisi ya Marekani inayopambana na uhalifu wa kifedha (FinCEN) kwa utakatishaji wa fedha haramu.

Kimsingi wananchi wa kawaida wanahitaji kujua usalama wa amana zao na kuambiwa ukweli kuhusu benki mbalimbali zinazofanya shughuli zake hapa nchini katika mazingira ya wazi wanayoweza kuyaelewa.