Mghwira Rais amekuamini chapa kazi

JUZI Rais John Magufuli alimwapisha Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Kilimanjaro, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Said Meck Sadick aliyeomba kujiuzulu na kukubaliwa.

Katika hafla ya kuapishwa huko, Rais Magufuli alieleza sababu za uteuzi wake kwa Watanzania mbalimbali, akisisitiza kuwa imetokana na uwezo wa kufanya kazi kuwatumikia Watanzania, na hasa uadilifu wake.

Rais alisisitiza kuwa anajua uteuzi huo, umezua mijadala mingi ndani ya vyama mbalimbali ikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, Rais alimtaka Mghwira kutosikiliza yasemwayo na watu, bali kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa katika kuwatumikia wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro bila ubaguzi wa namna yoyote, ama wa kidini, kikabila au kisiasa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Magufuli alimhakikishia Mghwira kuwa atampa ushirikiano wote unaohitajika katika kutekeleza majukumu yake.

Sisi tunasema, tunampongeza kwanza Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi unaozingatia zaidi maslahi ya taifa, na sio maslahi ya chama chochote cha siasa wala mtu binafsi. Tunasema mwendo huu utazidi kuliunganisha taifa na hatimaye taifa la Tanzania litakuwa na ajenda za pamoja kitaifa.

Kadhalika, tunampongeza Mghwira kwa kuteuliwa na kuapishwa, kuanza kazi sambamba na kauli aliyoitoa baada ya kuapishwa kuwa yeye si mpinzani wa maendeleo. Pamoja na hayo, tunapenda kumkumbusha Mghwira hatua ya kuteuliwa, inaonesha kuwa Rais ameridhika na uwezo wa kazi na uadilifu kwa taifa.

Kwa msingi huo, tunasema katu asiiangushe mamlaka ya uteuzi iliyomteua kwa kufanya mambo ‘ndivyo sivyo’ bali yaliyotarajiwa na aende mbali zaidi ya pale alipofikia mtangulizi wake ili Rais ajiridhishe kuwa hakukosea kumteua.

Tunasema, kwa kuwa vyama vya upinzani vipo ili kuchochea ushindani wa kimaendeleo, uwepo wao ndani ya Serikali sasa utimize azma hiyo kwa vitendo na kwa kushirikiana na watendaji wengine na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ili maendeleo yapatikane.

Tunaamini Mghwira hata wanachama na viongozi wengine wa upinzani, watakuunga mkono kwa dhati ili utende vizuri zaidi, kuonesha kuwa wapinzani wanaweza na Watanzania wote wanajenga nyumba moja ya Tanzania, hivyo hakuna sababu kugombea fito.

Hayo pamoja na mengine mengi, ndiyo yanatufanya tuseme Anna Mghwira, Rais John Magufuli amekuamini kwa niaba ya Watanzania, chapa kazi kumuonesha kuwa hajakosea kukuteua. Watanzania tunakuombea.