Ni bajeti ya maendeleo endelevu

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango jana aliwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa 2017/18 ya jumla ya Sh trilioni 31.7. Sisi tumeipitia vema na kubaini kuwa, ni bajeti iliyosheheni vipaumbele mbalimbali vya serikali katika malengo ya kuwafikisha Watanzania katika uchumi wa kati kupitia sera ya kukuza viwanda.

Bajeti hiyo ya pili kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imewasha moyo wa matumaini ya aina yake kwa ustawi na maendeleo endelevu ya nchi kwa jinsi ilivyokuwa inapokewa ndani na nje ya Bunge.

Hakuna ubishi kwamba bajeti hiyo imegusa maisha ya Watanzania wengi kutokana na ukweli kwamba mambo yaliwasilishwa yanagusa maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida.

Mambo mazuri yaliyomo ndani ya bajeti hiyo ni pamoja na kufuta ada ya kila mwaka ya leseni ya magari, kufuta ada ya ukaguzi wa viwango vya mazao ya biashara, kuondoa VAT kwa huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa na mizigo nje ya nchi.

Sambamba na hayo, bajeti hiyo imewatambua rasmi wafanyabiashara ndogo wasio rasmi maarufu kama machinga, mamalishe, wauza mitumba, kuondoa ushuru wa forodha kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumizi ya walemavu.

Sisi tunaipongeza serikali kwa kuwasilisha bajeti inayojali maslahi ya taifa pamoja na wananchi wake katika ngazi mbalimbali ili kujenga uchumi imara, endelevu na wenye kumwendeleza kila anayejitahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Kutokana na hali hiyo ya matumaini mapya kwa maisha na uchumi wa Watanzania, tunapenda kuwakumbusha wananchi wote kwa jumla kuwa, kila mwananchi kwa nafasi yake sasa achape kazi kwa manufaa yake binafsi, familia na taifa lake.

Yeyote anayetaka kula bila kufanya kazi sasa asipate nafasi kutokana na ukweli kwamba, mianya iliyokuwa inatumiwa na wajanja wachache kulihujumu taifa, sasa imezibwa na inaendelea kuzibwa.

Hatua sahihi zilizochukuliwa zimeonesha matunda mema ya kuongeza mapato ya uhakika na hali hiyo kuoneshwa kiuhalisia katika bajeti iliyowashwa. Tunasema tunaipongeza serikali kwa hatua za makusudi ilizochukua kukabiliana na wahujumu uchumi wa taifa letu katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi feki, vyeti feki na wanafunzi hewa.

Ni wazi kwamba mianya hiyo ya ufisadi iliyozibwa imetoa nafasi na ahueni kwa serikali kujipanga vyema na kwa uhakika kuiwezesha kuwasilisha bajeti inayowajali wananchi wake.

Tunasema huu ni wakati sasa kwa kila mmoja wetu kuchapa kazi ili kujihakikishia kwamba bajeti iliyowasilishwa inakuwa na manufaa kwa wananchi na serikali yao ili kujiletea maendeleo ya kweli na endelevu. Hongera serikali kwa bajeti yenye matumaini chanya kwa watu wake.