SportPesa iboreshe michuano

MICHUANO ya Kombe la SportPesa inatarajiwa kufikia tamati kesho katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam kwa mechi kati ya Gor Mahia na AFC Leopards zote kutoka Kenya. Wakati Gor Mahia imefikia fainali hiyo kwa kuwanyuka ndugu zao wengine, Nakuru All Stars, AFC Leopards iliwatoa wenyeji, Yanga.

Tunazipongeza timu zote zilizoshiriki michuano hiyo, Simba, Singida United na Jang’ombe ya Zanzibar kwa kuwa sehemu ya mashindano. Michuano hii imekuja wakati muafaka kwani ni muda ambao timu zimemaliza kucheza Ligi Kuu na zinajiandaa na usajili kwa ajili ya msimu ujao.

Ni wazi timu hizo zitakuwa zimenufaika na michuano hiyo kwa kutumia fursa hii kuwapima wachezaji zinaotaka kuwasajili au kupata waliong’ara. Mbali ya kupata wachezaji, timu zimepata pia zawadi ambapo mshindi atapata dola 30,000, wa pili dola 10,000 na zilizoingia nusu fainali, Yanga na Nakuru All Stars dola 5,000 kila moja.

Awali zote zilipewa dola 2,000 za maandalizi. Zawadi hizo ni motisha mkubwa kwa timu zote, hasa ukizingatia mzigo mkubwa ambao klabu zinao wa kusajili, kulipa mishahara ya wachezaji na kuendesha masuala mengine ya timu husika.

Ni matumaini yetu wadhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya michezo ya kubahatisha, SportPesa ya Kenya itaendelea kuandaa michezo hiyo na kuongeza zawadi kwa timu. Tunasema hivyo tukiamini kuwa SportPesa watakuwa wamepata faida ya kutangaza zaidi biashara yao kupitia michuano hiyo na hivyo wanaweza kuiboresha na kuongeza zawadi.

Kwa wenyeji, Yanga, Simba, Singida United na Jang’ombe ya Zanzibar tunapenda kuwapa pole kwa kutolewa mapema, lakini tunaamini hilo ni fundisho la kujiandaa zaidi mashindano yajayo.

Pamoja na changamoto za ukata, usajili, baadhi ya wachezaji wake kuitwa timu ya Taifa Stars inayojiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, bado tunadhani zingejipanga, zingefanya vizuri zaidi.

Haikuwa busara kwa timu hizo hasa Yanga na Simba, kuchezesha wachezaji wapya wa vikosi vya pili kwenye michuano mikubwa kama hiyo na bado zitarajie mafanikio. Kutolewa kwao kunapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na viongozi, wanachama na hata mashabiki kwani kunamaanisha kuinyima nchi, fursa ya kupata uzoefu wa kucheza na timu kubwa kama Everton inayokuja Julai 13, 2017.

Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England nayo inadhaminiwa na SportPesa na inakuja nchini kwa mwaliko wa kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha kwa lengo la kukuza soka nchini. Kwa Yanga na Simba kutolewa mapema, Tanzania imekosa fursa muhimu ya kujipima kiwango chake cha soka dhidi ya timu ya Ulaya na pia kunufaisha wageni, Kenya kwa mapato.

Wakati huu tunapouguza maumivu ya timu hizo kutolewa, ni wakati muafaka kwa viongozi wake kutafakari walipokosea na kurekebisha makosa yao ili michuano ijayo, makosa haya yasijirudie.

Ni matumaini yetu SportPesa watakuwa wamefaidika na hatua ya mashabiki wa soka nchini kuwaunga mkono kwa kujitokeza kwa wingi katika michuano hiyo mwanzo mwisho.

Hivyo, tunatarajia wataondoka wakiwa na furaha ya kufanikisha malengo yao na kuzidi kuvutiwa kuja kuwekeza zaidi biashara zao na kupanua wigo wa ajira na kuongeza mapato.

Kwa njia hiyo watakuwa wanaisaidia Tanzania na kukuza soka lake na kusaidia kuinua pia michezo mingine mtambuka kutokana na faida inayotokana na uwekezaji wa biashara zao. Tunaomba wananchi, mashabiki wote na pia viongozi wa Serikali waendelee kuwapa kila aina ya ushirikiano, kama waliouonesha kwa muda wote wa maandalizi na pia katika mechi.