Tushangilie bajeti kwa kuchapa kazi

ALHAMISI iliyopita Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha bungeni makadirio ya bajeti yake kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 takribani Sh trilioni 31.7.

Wakati bajeti ikiwasilishwa bungeni, wabunge na hata wananchi katika maeneo yao mbalimbali walikuwa wakishangilia kile walichokiona kuwa ni bajeti bora na hata baada ya hapo, wananchi wa kada mbalimbali wameendelea kuipongeza bajeti hii ya pili katika uongozi wa Rais John Magufuli.

Yapo maeneo mengi ambayo bajeti hii imepongezwa yakiwamo maendoleo na mapunguzo kadhaa ya kodi, hasa kuondolewa kwa kodi ya mwaka ya matumizi ya barabara kwa magari maarufu kama “Motor Vehicle Road Licence”. Kodi hiyo imehamishiwa katika manunuzi ya mafuta ya taa, dizeli na petroli kwa nyongeza ya shilingi 40 kwa lita.

Sisi tunaungana na Watanzania wengine kuipongeza bajeti hii iliyoandaliwa kwa umakini huku ikizingatia makundi mbalimbali ya watu wakiwamo wenye ulemavu ambao nao, wameondolewa kodi katika uingizaji wa vifaa wanavyotumia. Viongozi kadhaa wa watu wenye ulemavu wamenukuliwa katika gazeti hili wakiipongeza na kuishukuru Serikali.

Ubora wa bajeti ya mwaka huu umemsukuma Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Augustine Mrema, kusema sasa magereza yatapumua kwa kuwa wahalifu wengi wataachana na uhalifu na kuingia katika uzalishaji mali kwani fursa zimeongezwa wigo.

Wachumi na wasomi wanasema, hii ni bajeti inayoakisi nia ya Serikali kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda. Hii ni kwa kuwa bajeti imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji huku ikijikita katika kulinda soko la bidhaa na mazao ya ndani ya nchi.

Ndiyo maana sisi tunakiri na kuunga mkono tukisema, hii kweli ni bajeti ya watu. Hata hivyo, licha ya kuipongeza bajeti hii, yapo mambo kadhaa tunayoamini lazima tukumbushane kwa manufaa wote.

Ndiyo maana tunasema, wakati tukiendelea kuipongeza bajeti, tusiipongeze kwa maneno usiku kucha, mchana kutwa, bali tuipongeze kwa nyakati hizo zote huku tukifanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi ili maana ya bajeti hiyo bora ionekane kwa vitendo na uhalisi wake.

Tutakuwa tunajidanganya kama tutatumia muda wetu mwingi kukaa vijiweni au maeneo ya kazi tukisimulia, kusifia au kubishana kuhusu ubora wa bajeti, huku tukisahau wajibu wa kuitafsiri bajeti hiyo katika vitendo hasa ukizingatia imefungua na kupanua wigo wa fursa ya kila mmoja kufanya kazi na kuzalisha mali.

Tunasema hivyo tukizingatia kuwa, bajeti nzuri bila kufanya kazi, ni sawa na ndoto za mwendawazimu kutaka kujenga ghorofa hewani. Hili ndilo linatufanya tuseme, tuushangilie bajeti, lakini tukumbuke na kuzingatia kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.