TFDA ni kielelezo cha huduma bora kimataifa

MAABARA ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA ) imekuwa kielelezo cha utoaji wa huduma bora na kukidhi viwango vya kimataifa, hivyo kuifanya kuwa moja ya maabara zinazotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ubora, ambapo majibu yanayotolewa katika maabara hii yanatambulika kimataifa.

Ni katika utendaji huo, maabara ya uchunguzi wa chakula na ya maikrobaolojia, zimepata ithibati kwa kiwango cha Kimataifa ISO/IEC 17025:2005 baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Tuna kila sababu ya kujivunia taasisi hiyo kwa kuwa imekuwa mfano mzuri kwa utendaji barani Afrika kutokana na kutekelezwa kwa mfumo wa utoaji huduma (QMS) sanjari na mifumo ya kielektroniki.

Taasisi hiyo imefanikiwa kushika nafasi ya pili na kuwa ya mfano kwa uongozi na utendaji kati ya wizara, idara, taasisi na wakala zote za Serikali kwa mwaka 2010, 2011 na 2015. TFDA inastahili pongezi, sio kwa hayo tu, bali pia kwa kutambua changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika usajili wa majengo na bidhaa zao.

Kuwepo kwa mkataba wa maridhiano (MOU) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni kichocheo cha kukuza sekta ya viwanda hasa kipindi hiki tunapojenga na kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Mkataba huu unatambua mchango wa kila taasisi katika tasnia ya ujasiriamali wa bidhaa, zinazodhibitiwa na mamlaka na namna ya kupunguza gharama ya usajili. Aidha, TFDA itatumia matokeo ya TBS ya vipimo vya maabara kusajili bidhaa husika, ambapo TBS itazingatia usajili wa TFDA wa majengo na bidhaa wakati wa kutoa alama ya ubora.

Dhamira ya TFDA ni kutoa mafunzo kwa wasindikaji ili kuwajengea uwezo katika masuala yanayohusu usindikaji vyakula, ambapo wajasiriamali takribani 2000 wameshapatiwa mafunzo hayo tangu kuanzishwa kwa programu hii. Jambo hili ni ishara njema hasa wakati huu, ambapo Serikali inasisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Tumekuwa tukishuhudia wataalamu wakija kutoka mamlaka za udhibiti wa bidhaa za chakula kutoka katika nchi za Zambia, Botswana, Msumbiji, Burundi, Nigeria, Ghana, Cameroon, Ghana, Kenya, Ethiopia, Liberia, Rwanda, Sudani Kusini na Uganda, lengo likiwa kujifunza jinsi mamlaka yetu ilivyofanikiwa.

Jambo jingine la kujivunia ni kuwa TFDA imeteuliwa kuwa taasisi kiongozi katika kuandaa miongozo ya uwiano wa usajili wa dawa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hii ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa miaka mitano (2012-2016) wa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa.

Pia mamlaka hiyo imefanikiwa kupewa zabuni za kimataifa katika uchunguzi wa kimaabara kutoka nchi mbalimbali, kama vile Rwanda na Liberia. Tuna kila sababu ya kujivunia ushahidi huu, kwa kuwa Tanzania imepiga hatua katika kutoa huduma bora.

Ongezeko la wateja wanaoridhika na huduma kwa wateja wa ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2013/2014 ni ishara tosha kuwa mamlaka hii imepiga hatua kubwa kimataifa. Kiwango cha kuridhika kwa wateja wa ndani na nje, kimefikia asilimia 74.4 na 67, ukilinganisha na asilimia 63 na 66 mwaka 2008.