Maadhimisho mtoto wa Afrika yamkomboe mtoto wa Tanzania

KESHO Tanzania inaungana na nchi nyingine kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Juni 16 kama ilivyoazimiwa na nchi 51 za Umoja wa Afrika mwaka 1990. Kitaifa siku hii inaadhimishwa mkoani Dodoma ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi Na Fursa Sawa Kwa Watoto.”

Azimio hili lilipitishwa ili kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanyika katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini Juni 16, 1976. Utawala wa Makaburu uliwaua kikatili watoto waliokuwa wakidai haki ya kutokubaguliwa kutokana na rangi yao.

Kimsingi, kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza uzingatiaji wa jukumu la ulinzi wa mtoto na utoaji wa haki sawa kwa watoto wote ili kufikia maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030. Hata hivyo, wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine katika maadhimisho haya, Mtoto wa Afrika nchini Tanzania bado anamwaga chozi la damu kwa namna mbalimbali zinazotaka kutazamwa kipekee.

Nchini Tanzania bado kuna matukio ya kila mara ya watoto kunajisiwa, kubaguliwa, kutelekezwa, kupigwa, kuchomwa moto na wengine kunyimwa huduma za kijamii na kufanyiwa ukatili wa kukeketwa au kulazimishwa kuingia ndoa za utotoni.

Watoto wanashuhudia, ugomvi wa kufedhehesha katika familia zao na pia, wanashangaa namna viongozi wanaoaminiwa na taifa wanavyouza uzalendo wao na kulisaliti taifa kwa manufaa binafsi. Wanaona wanalishwa “matango pori” kimaadili kutokana na wayaonayo kwa wakubwa.

Ndiyo maana tunasema, watoto wote waangaliwe kwa uhalisia wao. Mila potofu na sheria kandamizi zitazamwe na kuondolewa ikiwamo Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayotoa nafasi kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa chini ya miaka 18.

Watoto wanaobakwa na kuathiriwa kielimu na kiafya au kijamii, wajengewe mazingira rafiki na fursa muhimu kuokoa maisha yao ya baadaye. Sisi tunasema, kila mtoto apate huduma na haki zote za binadamu ikiwamo haki ya elimu, aepushiwe mazingira hatarishi kama ajira hatari kwa watoto, kupigwa ovyo na kubakwa.

Shule za sekondari za wasichana zote ziwe na mabweni. Katibu Mkuu wa Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), Stella Jailos amewahi kusema kuwa, watoto wana machozi, lakini tofauti za kimaumbile, zinawafanya watoto wa kike na wenye ulemavu kuwa na machozi mengi zaidi wakiwamo wenye ulemavu wanaofungiwa ndani.

Tunasema, turejee na kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayotambua haki ya kila mtu wakiwamo watoto wote. Tuzingatie mwongozo wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na Sheria ya Mtoto ya Zanzibar ya Mwaka 2011.

Tunasema, ‘Maadhimisho haya ya Mtoto wa Afrika yamkomboe mtoto wa Tanzania.’ Kujihakikishia utekelezaji kwa vitendo azma hii muhimu kwa watoto wetu wa kike, kila mmoja wetu awe macho dhidi ya yeyote katika jamii yetu anayetaka kuendeleza mateso dhidi ya watoto wetu wa kike