Ndondo Cup iungwe mkono

MICHUANO ya soka ya Kombe la Ndondo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo Jijini Dar es Salaam ikishirikisha timu 32. Michuano hiyo imeandaliwa na Clouds Media na kudhaminiwa na Azam Media ambapo itakuwa inarushwa mubashara.

Mratibu wa michuano hiyo, Shafii Dauda alisema timu hizo 32 zimegawanywa katika makundi manane ya timu nne nne. Tunapenda kuwapongeza Clouds Media kwa kubuni na kuendesha michuano hiyo kwa zaidi ya miaka minne sasa ikilenga kuibua vipaji ambavyo havijaendelezwa.

Tunawapongeza pia Azam Media kwa kukubali kuidhamini na pia kuirusha mubashara ili watazamaji zaidi waione na kuongeza soko la wachezaji nje ya nchi. Michuano hiyo inaendeshwa wakati muafaka ambapo nchi inashiriki michuano ya Afrika ya timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.

Pia inafanyika wakati timu ya soka ya wakubwa, Taifa Stars ikiwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2019 nchini Cameroun. Na zaidi, inafanyika wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiunda timu mpya ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys baada ya ile iliyoshiriki fainali za vijana Afrika nchini Gabon kupandishwa na kuwa Ngorongoro Heroes.

Ni wazi michuano ya Kombe la Ndondo itasaidia kuibua vipaji vipya vya wachezaji chipukizi wanaoweza kuingizwa kwenye moja ya timu hizo, Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes na au Taifa Stars.

Tunaamini, kuna vipaji vingi vya wachezaji soka ambavyo havijaonekana kwa viongozi wa TFF na makocha ambavyo vingeweza kuongeza nguvu katika timu hizo za Taifa. Ni jukumu la wachezaji wa timu hizo 32 kutumia fursa hii vyema kuonesha uwezo, mbinu, maarifa, juhudi na ufundi wao wote ili miongoni mwao, tupate nyota wapya.

Wakifanya hivyo, wataipa michuano hiyo, heshima kubwa inayostahili achilia mbali kutoa burudani kwa watazamaji uwanjani na watakaofuatilia matangazo mubashara. Pia watajitangaza zaidi kisoka ndani na nje ya nchi na kufungua milango kusajiliwa na timu kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya soka Tanzania bara au ligi za nchi za nje.

Mbali ya hiyo, watachochea biashara ya matangazo kutoka kwa makampuni mbali mbali kuwekeza kwenye soka la mitaani ili kuwafikia pia, wananchi wa kawaida huko. Michuano ya Ndondo inakutanisha timu za mtaani ambako wananchi wengi hupenda kuangalia timu zinazofanya mazoezi na kucheza mechi katika maeneo wanakoishi.

Ni wazi michuano hii inaendeleza uhusiano mwema wa wananchi kupitia michezo na kuongeza ushirikishwaji katika maendeleo. Itoshe tu kusema pamoja na changamoto zilizopo, Ndondo inabaki kuwa kielelezo cha nia ya taasisi mbalimbali kushirikiana na TFF na Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam na mingine, kuendeleza soka.

Uendelezaji soka usiachwe kuwa mzigo wa TFF au Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pekee. Huu ni wakati muafaka wa wadau, taasisi, makampuni, mashirika na kila mtu kushiriki kwa njia moja au nyingine kuinua soka ili hatimaye siku moja tucheze fainali za AFCON au hata Kombe la Dunia.