Siku tano za JPM Sabasaba zitanufaisha wengi

JUZI Julai mosi, Rais John Magufuli alifungua rasmi Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Katika maonesho hayo, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) iling’ara kwa kuibuka mshindi wa pili katika tuzo ya vyombo vya habari vilivyoshiriki maonesho ya mwaka huu. Wakati wa ufunguzi, Rais Magufuli aliishauri Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan- Trade), kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa kiwanda cha mfano, badala ya kutumia fedha zake kujenga hoteli na majengo ya kisasa katika viwanja hivyo.

Mbali na ushauri huo kwa TanTrade, Rais pia aliishauri mamlaka hiyo kuongeza siku tano za maonesho ya mwaka huu katika viwanja hivyo ili Watanzania na wageni wengi wapate muda wa kutosha kuyatembelea kujifunza, kutangaza bidhaa na huduma zao, na wengine kupata fursa ya kutosha kununua bidhaa na mahitaji mbalimbali.

Watu wa kada mbalimbali wameonesha kufurahia ushauri huo wa Rais ambao Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade, Christopher Chiza, aliupokea na kutangaza nyongeza hiyo ya siku tano ya maonesho ya mwaka huu kama alivyoshauriwa na Mkuu wa Nchi.

Sisi tunasema, wazo na ushauri wa Rais Magufuli umekuja wakati mwafaka na umegusa matamanio ya wengi kwani uzoefu umeonesha kuwa, katika miaka ya nyuma, wengi wamekuwa wakilalamika kuwa, muda wa maonesho hayo yanayoanza Juni 28 hadi Julai 8, huwa hautoshi.

Tumekuwa tukishuhudia wananchi kadhaa wakilalamika kuwa muda unaotolewa, haukidhi mahitaji ya wengi hasa ikizingatiwa kuwa, siku mbili hadi tatu za mwanzo, bado huwa zinatumika kwa ujenzi na uandaaji wa baadhi ya mabanda.

Hali hiyo imekuwa ikiathiri msisimko wa maonesho haya muhimu kwa afya ya uchumi wa nchi katika pande zote yaani wageni wanaotembelea mabanda, pamoja na wafanyabiashara wanaotangaza huduma na bidhaa zao.

Ndiyo maana tunasema, pendekezo la Rais Magufuli la kuongeza siku tano za maonesho katika viwanja hivyo mwaka huu, litakuwa na faida nyingi kwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuongeza mauzo na manunuzi ya bidhaa mbalimbali, na hasa kupata fursa ya kutosha ya watu kujifunza katika maonesho hayo.

Ikumbukwe kuwa, maonesho ya mwaka huu yenye kaulimbiu isemayo, “Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda” yanazihusisha kampuni zipatazo 3,000 mbalimbali zikiwamo 515 kutoka nchi 30 duniani, hivyo ni fursa nzuri kila mmoja kupata nafasi ya kutosha kuyatembelea ili kufaidi huduma hizo.

Tunasema Tantrade watafakari umuhimu kujiandaa na kuandaa rasmi mazingira ili maonesho hayo yawe rasmi kwa siku zaidi ya hizi zilizokuwapo hadi Rais akalazimika kushauri nyongeza na ndiyo maana tunasema, “Siku tano za JPM Sabasaba zitanufaisha wengi.”