Tuache vyombo vya Dola vifanye kazi

TANZANIA imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote kwa kudumisha amani, mshikamano na umoja miongoni mwa watu wake bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa na kimakabila.

Msingi huo wa amani uliojengwa na kuimarishwa na Mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na kisha kuendelezwa na awamu zote za upongozi zilizofuata na hili sio siri, ni jambo la kujivunia kama taifa.

Tunasema ni jambo la kujivunia huku Watanzania tukimshukuru Mungu kwa kuwa ni rahisi kuipoteza amani, kuliko kuitafuta, kuipata, kuijenga na kuilinda ndiyo maana, kwa namna yoyote, hakuna apaswaye kulichezea “yai” hili.

Gharama za kuchezea amani tunaiona katika nchi mbalimbali zikiwamo baadhi ya majirani wetu na kwa msingi huo, ndiyo maana tunaunga mkono kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa juzi wakati akizindua Mradi wa Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam (DSMGP) alipowataka wanasiasa kuviacha vyombo vya dola kufanya kazi yake bila kuingiliwa.

Kauli ya Rais ina maana kuwa, kila mmoja bila kujali tofauti za kisiasa, kidini wala makabila, ana wajibu kuhakikisha anakuwa mlinzi wa kwanza wa amani ya nchi, sheria na kanuni zilizopo ili taifa liendelee kudumu katika tunu hii toka kwa Mungu isiyopaswa kuchezewa.

Hili litafanikiwa endapo pamoja na mambo mengine muhimu, vyombo vya dola vitaachwa vifanye kazi kwa weledi bila kuingiliwa. Tunasisitiza kuwa, ukiona vinaelea ujue vimeundwa, na hivyo, amani ya nchi haielei yenyewe bali inalindwa kwa gharama kubwa, hivyo, kauli ya Rais inaweka msisitizo wa uhalisia kuwa, iwe kwa kisingizio cha siasa, dini, harakati au kabila, hakuna anayepaswa kuachwa atumie kauli zinazoweka amani ya Watanzania rehani.

Sisi tunasema, kama alivyosema Rais, vyombo hivyo vinastahili kuungwa mkono kwa mawazo, maneno na hasa vitendo ili vitimize wajibu wa kulinda raia wa nchi na mali zao na sio kuvikatisha tamaa wala kufanya jaribio la kuviingilia kiutendaji.

Kila mmoja anapaswa kuchangia mbinu sahihi za kukomesha uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi za kuwezesha kuzuia uhalifu huo usitendeke na pia, kuwezesha wahalifu kutiwa mbaroni.

Kama ambavyo viongozi mbalimbali wamekuwa wakisisitiza akiwamo Amiri Jeshi Mkuu, kila mmoja ana wajibu kuhakikisha nchi inakuwa salama wakati wote kutokana na mchango na nafasi ya kila mmoja, na hii ndiyo sababu iliyomfanya kusisitiza wanasiasa waepuke kuviingilia vyombo vya dola.

Katika hili, kunahitajika mchango na wajibu wa kila mmoja kutambua nafasi yake muhimu katika kulinda na kuimarisha amani ya Tanzania. Tunaungana na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania kusema, vyombo vya Dola viachwe vifanye kazi zake na wanasiasa wasijaribu wala kupewa nafasi ya kuviingilia.