Tudhibiti wafugaji jeuri Bonde la Ihefu

MOJA ya habari katika gazeti letu la jana ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho “Korti kusogezwa Bonde Oevu la Ihefu”.

Kwa mujibu wa habari hiyo, serikali mkoani Mbeya imesema itahamishia mahakama katika eneo la Hifadhi ya Ruaha upande wa Bonde Oevu la Ihefu ili ifanye kazi maalumu ya kudhibiti wafugaji jeuri, wanaoingiza mifugo ndani ya hifadhi hiyo.

Moja ya kazi ya mahakama hiyo, itakuwa ni kutaifisha mifugo ya wafugaji watakaokaidi agizo la kutokuingiza mifugo hifadhini. Tunapongeza hatua hiyo, iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ambaye alisisitiza kuwa lengo la kuhamishia mahakama huko Ihefu, linatokana na baadhi ya wafugaji kuonekana kuwa sugu wa ulipaji faini kila wanapokamatwa, lakini hawaachi kuingiza mifugo hifadhini.

Ni wazi tabia hiyo ya wafugaji ni kero kubwa, ambayo haitakiwi kuvumiliwa tena na kiongozi yeyote au chombo chochote kile cha serikali. Kama wafugaji hao wa Ihefu wamekuwa sugu wa ulipaji faini, kinachotakiwa ni kubadilisha adhabu kwa kuweka adhabu kali zaidi.

Tunashauri kuwa baada ya mahakama hiyo mpya kuanza kazi Ihefu, pasiwepo na mfugaji yeyote mkaidi, atakayefumbiwa tena macho; na ikomeshe wafugaji wote wakaidi na mabingwa wa kulipa fidia.

Tumechoka na tabia hii ya kumtoza faini mfugaji asubuhi na analipa papo hapo kwa kuwa anazo fedha; na kisha jioni anaingiza tena mifugo katika hifadhi. Viongozi wote wa serikali kuanzia vitongoji, vijiji, kata, wilaya na mkoa, wasiwe tayari kuona ikolojia ya Ruaha inatishiwa na kusababisha uhalibifu wa Bonde la Ihefu na mto Ruaha kukauka.

Tunaomba wakazi wa vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Ruaha, kuendelea kutoa kutoa taarifa wanapoona wafugaji wasio waadilifu, wanaingiza mifugo hifadhini. Hali kadhalika, wakazi wa vijiji hivyo waache kufanya shughuli za kijamii hasa kilimo ndani ya mita 60 za kingo za mto Ruaha na mito mingine iliyopo eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa juhudi zilizoanza kuchukuliwa na serikali tangu mwaka jana, tayari zimeanza kuzaa matunda, kama vile baadhi ya wanyama wameanza kurudi katika eneo hilo. Hivyo, kamwe tusiwape nafasi watu wachache, ikiwemo wafugaji jeuri, kuharibu Bonde la Ihefu na Hifadhi ya Ruaha kwa ujumla.