Ndio! BMT ijipime kama inafaa kuwepo

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa wiki hii aliahirisha kikao cha saba cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma. Akiahirisha kikao hicho, aliagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia maudhui ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuona kama bado linakidhi haja ya kuwepo.

Alisema Serikali haitavumilia kuona usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa ukiendelea kudumaza michezo nchini. Tunampongeza Waziri Mkuu kwa kauli yake nzito iliyolenga kusafisha uozo ulioko michezoni tukiamini kuwa itachochea hatua ya kujisafisha.

Ni ukweli usiopingika kuwa, BMT kama taasisi ambayo inalea na kusimamia vyama mbalimbali vya michezo, imekuwa haiwajibiki ipasavyo. Badala yake, imebaki kama taasisi ya kupokea taarifa tu za yanayofanywa na vyama husika badala ya kuwa mstari wa mbele kuvisimamia.

Matokeo yake, viongozi wa vyama husika mara wanapochaguliwa hujigeuza miungu watu kwa kupanga safu zao kwa upendeleo wa dhahiri. Haiyumkiniki baadhi ya vyama hujisahau kiasi cha kufuja mapato na mali za wanachama wake kwa kuwa hakuna wa kuwanyooshea vidole.

Umefika sasa wakati wa BMT kujitafakari upya kama inafaa kuendelea kuwepo au ivunjwe na viongozi wapya wapewe dhamana ya kuongoza. BMT ndio chombo kilichoundwa na Serikali ili kusimamia na kuendeleza michezo. Iweje basi leo kikose nguvu ya kusimamia michezo hiyo.

Kwa mfano, inakuwaje inaruhusu vyama vya michezo kutengeneza katiba zinazokinzana na Katiba ya nchi kwa kutotendea haki watu wote. Inakuwaje BMT inabaki kama mgeni mwalikwa wakati viongozi wa vyama husika wakiendesha mambo ndivyo sivyo kwa kupindisha sheria.

BMT inatakiwa kujua kuwa, hakuna taasisi ya michezo iliyo juu ya sheria za nchi hata kama ina matawi au uhusiano na taasisi za kimataifa. Ni matumaini yetu kuwa, agizo hili la Waziri Mkuu litatumika kama dira ya viongozi wa BMT kurekebisha upungufu uliopo ndani ya baraza.

Kama tatizo ni sheria, sera au miongozo, ni vyema viongozi wakaipitia upya na kushauri Serikali kupitia Bunge au Wizara, zibadilishwe. Kwa mfano, hatuoni mantiki ya Msajili wa Vyama vya Michezo nchini kushindwa kufanya kazi na BMT kuvibana vyama vyenye ukiritimba.

Inashindikanaje kwa mfano Msajili kuvibana vyama visivyofanya ukaguzi wa hesabu zake hata kama mapato yake hayatokani na Serikali. Tunasema hayo kwa sababu pamoja na vyama vingine kutotegemea fedha za Serikali, bado vina dhamana kubwa kwa Watanzania wote.

Kwa maana hiyo, si haki hata kidogo vyama hivyo kukataa kudhibitiwa katika uendeshaji wakati maslahi ya michezo vinayoisimamia ni ya wananchi wote hata kama si wanachama wake.

Ifike wakati vyama husika vijue kuwa, usajili vinaopewa haumaanishi kuwa ni wa kundi hilo dogo la wanachama bali ile ni dhamana tu wanayopewa kuisimamia kwa niaba ya wote.