Hospitali za umma zimulikwe

SERIKALI imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa muda mrefu sasa, kuboresha huduma za afya nchini na mojawapo ni kukomesha ukosefu wa dawa mbalimbali.

Mathalani, juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangaza kuwa tatizo la dawa nchini, sasa litakuwa ni historia kutokana na Bohari ya Dawa Nchini (MSD) kuanza kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.

Kwamba hatua hiyo itafanya upatikanaji wa dawa, uwe kati ya asilimia 90 na 100 kuanzia mwaka huu wa fedha. Pia hatua ya kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, itapunguza gharama za kununua dawa na zitashuka bei kwa kiasi kikubwa cha kati ya asilimia 15 na 80.

Mabadiliko haya ya bei, yataleta unafuu mkubwa kwa wananchi kuanzia mwezi huu. Ni wazi kuwa dawa muhimu 135 kwa hapa nchini, zitapatikana wakati wote katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za serikali, jambo ambalo litawafanya wananchi kuhudumiwa vizuri.

Kwa mujibu wa Ummy, hatua ya MSD kuanza kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuitaka serikali iagize dawa kutoka kwa wazalishaji, bila kupitia kwa madalali.

Lakini wakati serikali ikiboresha upatikanaji wa dawa, kwa upande mwingine hali ya utoaji huduma katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma, inasikitisha na kutia uchungu, kwa mfano Hospitali ya Sinza Palestina iliyopo wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, yeye ni miongoni mwa waathirika wa huduma mbaya na manyanyaso wanayofanyiwa wagonjwa na hata wafiwa katika hospitali mbalimbali nchini, ikiwemo hospitali hiyo ya Sinza Palestina.

Waziri huyo anaeleza kwamba mwili wa marehemu kaka yake, ulitupwa kwenye gari kama mzoga, ulipokuwa ukipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, wilayani Kinondoni.

Simbachawene aliyekuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya mjini Dodoma, anawataka waganga hao wakuu kuchukua hatua kali, ikiwemo kuwafukuza kazi watumishi wanaonyanyasa wagonjwa ili kukomesha tabia hiyo ambayo inachafua sekta ya afya nchini.

Pia anataka Hospitali ya Sinza Palestina iangaliwe kutokana na kukithiri kunyanyasa wagonjwa na hata miili ya watu waliofariki pindi wanapotaka kuchukuliwa na ndugu zao, ambapo wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa ndugu wa marehemu, hali ambayo imekuwa ikizidisha uchungu mara mbili.

Anasema ni jambo lisilokubalika kuona baadhi ya watumishi wachache, wanaendelea kuichafua sekta ya afya bila kuchukuliwa hatua. Hivyo, tukio hilo la Sinza Palestina linadhihirisha kwamba kwenye sekta ya afya nchini, bado kuna watumishi wabaya ambao wanachafua sekta hiyo nyeti.

Kutokana na hali hiyo, kwanza tunawashauri viongozi wa kisiasa, mfano madiwani, wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa, kutembelea mara kwa mara zahanati, vituo vya afya na hospitali katika maeneo yao na kujionea uozo uliopo katika maeneo hayo.

Hali kadhalika, wafanye mikutano na wananchi na kuwauliza juu ya utoaji huduma wa madaktari na wauguzi katika maeneo yao. Tuna hakika wananchi hawawaogopi watumishi wazembe, wanyanyasaji na wanaotoa lugha chafu kwa wagonjwa, hivyo watawataja kwa majina na kuomba wachukuliwe hatua kali.

Nanyi viongozi wa wizara ya afya, fanyeni ziara za mara kwa mara za kushtukiza katika zahanati, vituo vya afya na hospitali, kukagua utendaji kazi wa maeneo hayo