Agizo la Waziri litekelezwe

HABARI kwamba Serikali imesitisha uchimbaji na uchotaji wa mchanga kiholela katika maeneo yasiyo rasmi ni taarifa njema hasa kwa wanaoishi katika maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na uchimbaji huo ambao umekithiri katika Jiji la Dar es Salaam na kwingineko nchini.

Uchimbaji huo mbali na kuondoa tabaka la juu ambalo ndilo lenye rutuba kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo, umekuwa ukiharibu mandhari ya maeneo husika. Pia umekuwa ukisababisha uharibifu mkubwa wa uso wa dunia na kufanya maeneo ambayo yamevamiwa na wachimbaji kuwa si rafiki kwa maisha ya viumbe hai wakiwemo wanyama, mimea na wadudu.

Akiwa katika ziara yake ya kutembelea Mto Nyakasangwe uliopo maeneo ya Boko kata ya Bunju, Dar es Salaam juzi, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina alisitisha uchimbaji na uchotaji wa mchanga kiholela katika maeneo yasiyo rasmi.

Jiji la Dar es Salaam limeathirika sana na uchimbaji huu. Maeneo ni mengi karibu kila wilaya. Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri wana kazi kubwa ya kufanya katika Awamu hii ya Tano ya Rais John Magufuli ambayo moja ya sifa zake ni kuondoa uozo katika jamii.

Malori mamia kwa mamia yamekuwa yakisomba mchanga maeneo mengi ambayo hayajalengwa kwa biashara hiyo na vijana wamekuwa wakichimba hata maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii. Wakati mwingine wanavamia mashamba ya watu kwa vitisho wakitishia maisha ya wahusika.

Yametokea sana maeneo ya Bunju na kwingineko, lakini wahusika wamekaa kimya. Ni kutokana na hali hiyo aliyoiona Waziri Mpina akatoa siku 30 kwa Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kubaini na kutenga maeneo ya uchimbaji ya mchanga ambayo yapo ndani ya manispaa zao.

Akasema kuna maeneo ambayo wananchi wanaweza kufika kwa urahisi, Manispaa zinapaswa kuyatembelea maeneo hayo na kuyabaini kama kuna uwezekano wa kuchimba mchanga.

Mpina akaongeza kwamba ndani ya mwezi mmoja, manispaa hizo zinatakiwa kuandaa utaratibu mfupi wa kutenga maeneo hayo ikiwemo utoaji wa vibali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Halmashauri pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Tunatamani agizo la Waziri Mpina lifanyiwe kazi na wahusika sasa. Pia tumuombe isiishie katika Mto wa Nyakasangwe uliopo maeneo ya Boko, bali baada ya muda atembelee na maeneo mengine aone uharibifu huu wa mazingira kutokana na wachimbaji kuharibu uoto wa asili kiholela na kuona kama agizo alilotoa juzi limetekelezwa na wahusika wanachukuliwa hatua.