Simba, Yanga zijifunze Everton kuhusu Ukimwi

TUME ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) imesema imeandaa tamasha maalumu la kuchangisha fedha za kuendesha Mfuko wa Wakfu wa Ukimwi mkoani Mbeya.

Habari za tamasha hilo zilitolewa kwanza na Mkurugenzi wa TACAIDS na kisha juzi kurudiwa na Mkurugenzi wake wa Sheria. Walisema wamezialika Yanga na Simba za Dar es Salaam kucheza mechi ya kirafi ki na timu za Mbeya City na Tanzania Prisons za Mbeya uwanja wa Sokoine.

Viongozi hao walisema Yanga itacheza na Mbeya City Julai 27, Simba na Tanzania Prisons, Julai 28 na Julai 29, itakuwa fainali. Viongozi hao wanasema tamasha hilo pia litaambatana na burudani mbalimbali za wasanii, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wa Mbeya kuchangia mfuko huo.

Mbali ya tamasha hilo, kutakuwa pia na harambee ambayo wananchi wa Mbeya na nchi nzima wanakaribishwa kuchangia siku ya mwisho na kupitia simu 0786909090. Tunawapongeza viongozi hao kwa kubuni tamasha hilo kuchangia shughuli za Ukimwi na pia kuwahusisha wanamichezo.

Timu za Yanga, Simba, Mbeya City na Tanzania Prisons ni sehemu ya jamii ya wanamichezo na Watanzania hivyo zina wajibu wa kuchangia harambee hiyo kwa wachezaji wake kuonesha vipaji vyao.

Ni wazi fedha zitakazopatikana katika mechi na kwenye harambee zitawezesha TACAIDS kuhudumia mamia kwa mamia ya waathirika wa HIV na UKimwi ambao miongoni mwao ni pamoja na wanamichezo.

Ndio maana tunasema iko haja kwa kila mdau wa soka Mkoa wa Mbeya na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kuangalia mechi hizo ili kwa njia hiyo wachangie. Uchangiaji wa shughuli za jamii nchini unapaswa kuhusisha pia wanamichezo kwani nao ni sehemu ya jamii yetu.

Kwa timu ambazo hazikuwa na programu kama hizo, tunaomba wajifunze kupitia tamasha hili na pia kupitia ziara ya Everton walipokuja nchini hivi karibuni. Everton walipokuja kucheza na Gor Mahia ya Kenya katika mechi ya kirafi ki ya Kombe la SportPesa, walipowasili nchini wachezaji wake waligawanyika mafungu mafungu kufanya shughuli za jamii.

Baadhi walienda shule ya msingi ya walemavu Uhuru Mchanganyiko, Ilala huku wengine wakienda kucheza soka na walemavu wa ngozi, Albino United FC. Everton walifanya yote haya kwa kujua kuwa wachezaji na hata klabu yao ni sehemu ya jamii ya Waingereza na hivyo wanao wajibu kusaidia shughuli za jamii ambazo Serikali na taasisi zake inasaidia.

Kama Everton ambayo inatoka nchi iliyoendelea wachezaji wake wanashiriki shughuli za jamii kama za kutembelea na kusaidia wanafunzi walemavu na albino, vipi klabu zetu kubwa kama Yanga na Simba zisijitoe kwa hali na mali kusaidia.

Itoshe tu kusema kuwa tatizo la Ukimwi si la mtu mmoja, ni la Watanzania wote, wazima na wagonjwa hivyo itakuwa vyema kama kila mmoja kwa kipaji chake, elimu yake, uwezo wake, akashiriki kuudhibiti. Kwa viongozi wa TACAIDS, tunaomba fedha zitakazopatikana zitumiwe vyema kwa maslahi mapana ya kudhibiti Ukimwi na kufi kia lengo lao la uwiano wa 909090.