Wenye vituo vya mafuta wasisubiri rungu la serikali

SERIKALI ya Awamu wa Tano inajitahidi kukusanya kodi na mapato mbalimbali ya serikali, kwa sababu fedha hizo ndizo zinazotumiwa na serikali kugharimia miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, pamoja na lengo zuri la serikali, bado wapo Watanzania wachache wanaosuasua kutekeleza wajibu wao, ikiwemo baadhi ya wenye vituo vya mafuta kushindwa kufunga mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs). Hatua hiyo ilisababisha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kufunga baadhi ya vituo hivyo hivi karibuni.

Karibu vituo 700 vya mafuta vilifungwa nchi nzima tangu kazi ya kuvikagua kama vimefunga EFDs ilipoanza. Lakini, tayari vituo 500 vimefunguliwa, baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na TRA na vingine 241 havijafunguliwa kutokana na kushindwa kukidhi masharti ya TRA.

TRA imelazimika kuendesha kampeni hiyo, baada ya kuwapo makubaliano na wafanyabiashara hao ya kufunga mashine hizo tangu mapema mwaka jana, lakini wengi walikaidi. Hivyo, kwanza tunaunga mkono hatua ya TRA ya kuvifungia vituo hivyo vilivyokaidi.

Pili, tunaunga mkono agizo lililotolewa Julai 19, mwaka huu na Rais John Magufuli ambapo ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta nchini, kuhakikisha kwamba wanafunga mashine za EFDs, ambapo sasa zimebaki siku kumi.

Rais anaonya kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo, watahatarisha biashara zao na anawataka wakuu wa mikoa na wilaya, kufuatilia na kusimamia jambo hilo kwa karibu. Alitoa agizo hilo alipohutubia mkutano wa hadhara mjini Biharamulo mkoani Kagera wakati wa kuzindua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga yenye urefu wa kilometa 154, ambayo itaifungua Tanzania na nchi za jirani katika Ukanda wa Magharibi.

Rais anasema kwa muda mrefu baadhi ya wafanyabiashara nchini, wanaoendesha vituo vya mafuta, wamekuwa wakikwepa kodi. Hivyo, anaiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini, vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo, vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

Kwa mujibu wa Rais, serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma muhimu ikiwemo afya na elimu, lakini kwamba haiwezi kufanikiwa katika masuala hayo, kama baadhi ya wafanyabiashara wanakwepa kulipa kodi na kuacha mzigo mkubwa kwa watumishi wa umma na wakulima kwa miaka yote.

Ni wazi kuwa TRA ilifanya ukaguzi wa muda mrefu kwenye vituo vya mafuta nchini ili kujiridhisha vinavyotumia na visivyofunga mashine hizo. Pia, jambo lingine dhahiri kwamba wenye vituo vya mafuta, walipewa muda wa kutosha, kufunga mashine hizo, lakini wengi hawajafunga hadi sasa.

Aidha, tumevutiwa na kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Phillip Mpango kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi; na kwamba katika suala la matumizi ya mashine za EFDs, serikali haina utani na mtu yeyote, ikiwemo wenye vituo vya mafuta.

Mpango anaonya wenye vituo vya mafuta, waache kukaidi kufunga EFDs na kuacha kusubiri siku 14 ziishe. Anawataka wasije kulalamikia hatua zitakazochukuliwa na serikali siku hizo zitakapokwisha, kwani yeye atasimamia kwa asilimia 100 agizo hilo lililotolewa na Rais Magufuli.

Anasema wale waliozoea kuichezea serikali, waache mchezo huo mara moja, badala yake wafanye kazi kwa pamoja na serikali na kutii maagizo yote wanayopewa. Mpango anasema malumbano yasiyo na tija, yanayofanywa sasa na baadhi ya watu kwenye magazeti na vituo vya televisheni kuhusu suala la EFDs, hayana tija na yaachwe mara moja.

Hivyo, tunawasihi wenye vituo vya mafuta, ambao hawajafunga mashine hizo, kutii agizo hilo la serikali ndani ya muda uliotolewa, ambapo kwa sasa zimebakia siku 10 tu.