Hongera TOC kuizawadia timu iliyoshiriki Madola

TIMU ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya Sita ya Jumuiya ya Madola kwa vijana na kutwaa medali ya shaba ilirejea juzi jijini Dar es Salaam ikitokea Bahamas na kupata mapokezi makubwa.

Tanzania katika michezo hiyo iliwakilishwa na wachezaji wanne wa timu za riadha na kuogelea na mwanariadha Francis Damas ndiye aliyoitoa kimasomaso nchi kwa kutwaa medali hiyo ya shaba.

Damas alishika nafasi ya tatu katika mchezo wa mbio za meta 3,000 kwa kutumia dakika 8.37.51 akimaliza nyuma ya Mkenya na Mcanada waliomaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili.

Timu hiyo ilipotua katika Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) walipokewa na viongozi na wadau mbalimbali wa michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

Timu hiyo baada ya kutua ilikwenda moja kwa moja katika Uwanja wa Taifa katika ukumbi wa VIP, ambako kulikuwa na hafl a fupi ya kuwapokea na kuwapongeza wachezaji hao pamoja na makocha wao, Mwinga Mwanjala (riadha) na Ameir Abdalla (kuogelea).

Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) iliwazawadia wachezaji na makocha hao, ambapo Damas alipewa sh 750,000 wakati makocha kila mmoja aliondoka na sh 400,000 wakati wachezaji waliobaki kila mmoja alipata sh 300,000.

Fedha hizo ambazo ni mbali na posho zao za safari, zilitolewa na TOC kama ahsante kwa wachezaji na makocha hao walioiongoza timu hiyo na kutwaa medali hiyo ya shaba. Ni jambo la kuipongeza TOC kwa kutoa fedha hizo kwani jambo lililofanywa na Damasi ni kubwa kwani Tanzania kwa mara ya mwisho ilitwaa medali kama hiyo mwaka 2008 Pune, India kutoka kwa Mary Naali.

Fedha hizo pamoja na kuwa si nyingi, lakini sio haba kwani zitawaongezea ari wachezaji ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kama hayo au mengine. Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika michezo mbalimbali ukiwemo riadha, soka na mingine, hivyo wakati umefi ka wa kuwatia moyo wachezaji wetu ili waendelee kufanya vizuri katika mashindano mengine.

Wiki ijayo mashindano ya dunia ya riadha yanatarajia kuanza London, Uingereza na Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshiriki mashindano hayo. Ni matarajio yetu makubwa kuwa matokeo ya Bahamas yataisaidia sana timu yetu itakayoshiriki mashindano London kufanya vizuri ili kuitangaza vizuri nchi kimataifa.

Mashindano ya dunia ni makubwa na magumu na Tanzania hadi sasa tuna medali mmoja tu kutoka kwa Christopher Isegwe baada ya kutwaa medali ya fedha katika mashindano yaliyofanyika Helsinki, Finland 2005.

Timu hiyo itawasili kesho Jumapili jijini Dar es Salaam na kuagwa Jumatatu, ambako itakabidhiwa bendera na Jumanne kuondoka kwenda London tayari kwa mashindano hayo, ambayo yataanza Agosti 5 hadi 13. Kila la heri timu ya Tanzania mashindano ya riadha ya Dunia.