Tuache uongo dhidi ya Tume ya Uchaguzi

KWA muda mrefu sasa Chama cha Wananchi (CUF) kimekuwa kwenye mgogoro, hivyo kugawanyika makundi mawili; moja ni la Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba na lingine linamuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad.

Mgawanyiko huo ulipamba moto hivi karibuni baada ya Profesa Lipumba kuamua kuwavua uanachama wabunge wanane kwa tuhuma za makosa kadhaa, hivyo kuiruhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuteua wengine wapya.

Lipumba anasisitiza kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho, na kwamba maamuzi yoyote yanayofanyika chini yake ni halali, kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Lakini, kwamba hatambui vikao vyovyote vya chama hicho, vinavyofanyika nje ya ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Buguruni Dar es Salaam, ikiwemo vikao vya Baraza Kuu la Taifa la Uongozi, vinavyofanyika chini ya Maalim Seif, bila yeye.

Profesa huyo anasema Maalim Seif hajafika ofisini Buguruni tangu Septemba 23, mwaka jana. Hivyo, anamtaka sasa Maalim Seif arejee ofisini kwao Buguruni na kwamba yupo tayari kumpokea.

Nalo Baraza Kuu la Taifa la Uongozi la CUF, lililokaa hivi karibuni chini ya Maalim Seif, lilisema wabunge hao 8 walioteuliwa na NEC, hawamo katika orodha waliyopeleka Tume. Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono taarifa ya NEC kukanusha madai yaliyotolewa na wiki iliyopita na Baraza Kuu la Taifa la Uongozi wa CUF kuhusu NEC kukiuka kanuni katika uteuzi wa wabunge hao wanane.

Taarifa ya NEC inasisitiza kwamba madai hayo ya CUF ni ya uongo na yanalenga kupotosha umma kuhusu utekelezaji wa kazi za tume hiyo. Ni dhahiri kwamba NEC imefanya uteuzi wa wabunge hao wanane, kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo CUF ndicho kilichopendekeza na kuwasilisha NEC majina ya nani ateuliwe kuwa mbunge wa viti maalumu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge hao wanane wa Viti Maalumu walioteuliwa, wapo kwenye orodha ya CUF iliyowasilishwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwa mujibu wa Tume hiyo, CUF ndiyo inajua ni nani siyo mwanachama wa chama hicho wakati wa kipindi cha kujaza nafasi wazi inapotokea; na kwamba majina hayo manane yaliyopendekezwa na CUF, kujaza nafasi wazi ya wabunge wa viti maalumu, ni miongoni mwa majina 55 yaliyowasilishwa NEC kwa barua ya CUF ya Septemba 28, 2015, iliyosainiwa na Maalim Seif mwenyewe. Hivyo, tunasisitiza kuwa tuiache NEC ifanye kazi zake.

Tuache uongo na tuache kuisingizia Tume. Vyama vya siasa vyenye migogoro, havina budi kwanza kutatua matatizo yao ya ndani, badala ya kuchafua jina, sifa na kazi nzuri ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.