Benki ziheshimu agizo la Makamu wa Rais

WIKI iliyopita Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alizindua Jukwaa la Uwezeshaji la Wanawake la Dar es Salaam. Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais alizitaka taasisi za kifedha zikiwamo benki, kuweka masharti nafuu na maalumu kwa wanawake wajasiriamali wadogo ili wengi wanufaike zaidi na uwepo wa mikopo hiyo.

Akasisitiza kuwa inashangaza kuona taasisi hizo zinatoza riba kubwa katika mikopo ya wanawake wajasiriamali, lakini zikiweka riba ndogo katika amana. Alizitaka benki zote nchini, kufanya kazi kwa maendeleo ya watu wote.

Kikubwa na cha kutia moyo kama ukombozi kwa wanyonge, Makamu wa Rais akaziagiza taasisi hizo za fedha zikiwamo benki, kurekebisha mifumo yao haraka ili ziwe na masharti nafuu na maalumu ya mikopo kwa ajili ya wanawake wajasiriamali wadogo.

Alikwenda mbali na kuwataka wananchi hasa wanawake, kutumia mazingira wezeshi na fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi na kimaisha na kuachana na maneno yasiyo na tija.

Sisi tunampongeza na kumshukuru Makamu wa Rais kwa kuzingatia adha wanazopata wanawake katika taasisi za fedha ikiwa ni pamoja masharti magumu ya kupata mikiopo, riba kubwa na hata kero ya kulazimika kufanya marejesho kila siku tena kwa kuhudhuria.

Tunasema mambo hayo, badala ya kuwa na nafuu kwa wanawake na wajasiriamali wengine, yameonekana kuwa kero kwa jamii, kwani urejeshaji mikopo wa kila wiki kwa taasisi za kifedha, unatumia muda mwingi na gharama za wajasiriamali.

Gharama hizo ukiwamo muda mwingi unaopotea, nauli na mahitaji kama chakula cha mchana ni vitu ambavyo vingetoa muda wa wanawake na wajasiriamali hao kuzalisha zaidi ili kuongeza tija.

Sisi tunasema, utaratibu wa shinikizo la taasisi hizo, kuwataka wakopaji ambao ndio wateja wao kufanya marejesho kila wiki tangu wiki ya kwanza ya mkopo, ukubwa wa riba licha ya masharti magumu, ndiyo umewafanya wanawake wengi wanaoingia katika mikopo kujikuta wanajiona kama watumwa wa mikopo, badala ya kupata nafuu katika maisha.

Wanawake wajasiriamali wawekewe mazingira na masharti nafuu ya ukopaji huku kama alivyoagiza Makamu wa Rais, riba wanayotozwa wanapokopa itazamwe upya na muda wa marejesho urekebishwe.

Tunasema, taasisi zote zikiwa na utaratibu wa marejesho kwa njia ya kielektroniki, mikopo itawanufaisha wanawake, badala ya hali ilivyo sasa ambapo wengi wanaelekea kuiona kama kitanzi.