Magereza, JKT waungwe mkono ujenzi ofisi za walimu

KESHO kutwa vijana 300 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na wafungwa wa magereza, wataanza ujenzi ofi si 402 za walimu mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ujenzi huu unatokana na mazungumzo yake na walimu wa shule za msingi na sekondari, waliobainisha uhaba wa ofisi kama kero kubwa katika kazi zao.

Walimu walimweleza kuwa uhaba au uduni wa ofisi shuleni, ni kero inayopunguza morali ya kazi yao, na kuleta matokeo duni ya kitaaluma yasiyofurahisha. Makonda anabainisha hayo wakati akitambulisha Kamati ya Ujenzi wa Ofisi hizo kwa shule za msingi na sekondari, itakayoongozwa na Kanali Charles Mbughe JKT akiwa Mwenyekiti.

Ujenzi huo utafanywa chini ya vyombo vya ulinzi na usalama kutoka JKT, ambao tayari wametoa vijana 300 kwa ajili ya ujenzi wakishirikiana na Jeshi la Magereza, litakalotoa wafungwa watakaosaidia kufyatua matofali. Sisi tunasema, ushikwapo shikamana.

Wazo la ujenzi wa ofisi za walimu katika shule zetu ili walimu wafanyie kazi katika mazingira mazuri ni muhimu kwa manufaa ya watoto wetu na hatimaye taifa zima. Kwa msingi huo, ubunifu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hauna budi kuigwa na kuungwa mkono na wapenda maendeleo wote nchini.

Ndiyo maana tunasema, kwa kuwa tayari mafundi watapatikana na hata wafyatua matofali wenye ufundi na uzoefu, ni wajibu wetu wananchi kuchangia kwa hali na mali kufanikisha mpango huu.

Tunasema, hata mpango huu utakapokamilika, usiishie tu kwa ofisi za walimu, bali pia huduma muhimu kama vyoo vya kutosha na vya kisasa kwa shule zetu. Hili nalo likifanyika, litatoa uhakika kwa vijana wetu wawapo shuleni, kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na uhaba au uduni wa vyoo unaowafanya wengine, kuamua kujisaidia vichakani, jambo ambalo ni hatari zaidi.

Ndiyo maana tunasema, tunapaswa kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa michango mbalimbali ikiwamo ya fedha au vifaa mbalimbali vya ujenzi kama mabati, nondo, saruji, kokoto, mchanga, mbao, misumari na hata nguvu kazi ya watu ili kufanikisha haraka suala hili muhimu.

Hili sasa, litujengee utamaduni wa kupenda kuchangia mambo ya maendeleo kwa jamii, kuliko kuchangia tu, sherehe. Ndiyo maana tunasema, ujenzi wa ofisi za walimu Dar, uwe mfano nchini na uungwe mkono.