Tukabiliane na uhaba wa madarasa kwa vitendo

HABARI kwamba wanafunzi 49 wa Shule ya Msingi Kizerui wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wanasomea chini ya mti, bado zinaendelea kugonga vichwa vya wapenda mazingira bora ya kutolea elimu nchini.

Tunapongeza hatua za awali zinazochukuliwa na Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela kwa kuanzisha kampeni ya michango kupata fedha za kujenga madarasa kwa ajili ya kuwaokoa wanafunzi hao kutoka katika kadhia ya kuketi chini ya mti, wakifuatilia masomo.

Katika kampeni hiyo, tayari zaidi ya Sh milioni moja zimechangwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili. Sisi tunataka kutoa mwito kwa viongozi wa siasa, serikali na jamii kutumia habari hii, kama changamoto ya kutukumbusha kwamba kampeni ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa, madawati na nyumba za walimu kwa shule zetu za msingi na sekondari za serikali bado lipo.

Hapa tungependa kuwakumbusha wenye dhamana katika sekta ya elimu katika ngazi ya kata, wilaya na mkoa, kufanya tathmini ya mahitaji hayo kupata kiwango kilichofikiwa na kampeni hiyo kitaifa katika kila shule ili kubaini uhaba uliopo na kuendeleza juhudi za kukabiliana nayo kwa vitendo.

Tunaamini hatua hiyo ya kufanya tathmini, itaweza kutoa mwanga wa kubaini shule nyingine zenye tatizo linalofanana na la shule hiyo ya Same, ili kuchukua hatua stahiki za kulipatia ufumbuzi.

Hakuna ubishi kwamba elimu ni msingi wa maisha na haki ya kila mtoto, lakini ni ukweli pia kwamba haina budi kutolewa katika mazingira rafiki, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa madarasa na viti vya kukalia wanafunzi na walimu wao.

Serikali ya Awamu ya Tano ilifuta ada kwa shule zote za msingi na sekondari za serikali tangu mwaka jana kwa lengo la kuwapunguzia wazazi mzigo wa kugharimia elimu kwa ngazi hizo na kuwanusuru watoto wengine, waliokosa kwenda shule kwa sababu ya kukosa ada, nao wapate fursa hiyo muhimu katika maisha yao.

Katika hali hiyo, tanapenda kuwakumbusha wazazi na walezi kwamba suala kwa mfano wa ujenzi wa madarasa, halina budi kusubiri na badala yake wananchi kupitia kwa viongozi wao katika eneo lao wahamasishwe kuchangia au kushiriki kutoa nguvu kazi kwa ujenzi wa madarasa, badala ya kusubiri kuonewa huruma.

Kama serikali imechuka hatua za makusudi kuondoa ada, kwa nini kwa upande wa wazazi na walezi, wasichukue hatua za kukabiliana kwa vitendo tatizo la ukosefu wa madawati na viti kwa kuchangia kuokoa watoto wetu katika kadhia kama hiyo. Hili linawezekana, tuamke kukabiliana nalo.