Uchaguzi Chaneta urejeshe heshima ya netiboli nchini

UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) unafanyika leo mjini Dodoma, huku ukitarajiwa kuwapata viongozi watakaoongoza kwa miaka minne ijayo.

Kufanyika kwa uchaguzi huo ni sehemu ya kutekeleza kipengele cha Katiba ya Chaneta kinachotaka kila baada ya miaka minne, kufanyike uchaguzi ili kupata viongozi wapya au kuhalalisha wale wa zamani kama wamegombea.

Uchaguzi huo unafanyika kwa usimamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo nalo lina dhamana ya kuhakikisha vyama au mashirikisho ya michezo vinaendeshwa kwa kufuata katiba zao.

Tayari wadau wa michezo wakiwemo wengi wa viongozi waliopita wa Chaneta wamechukua fomu na kuzirejesha wakitaka kuongezewa muda wa kuongoza chama hicho. Karibu wadau wote wanaowania nafasi hizo wanasema wanataka kuupa uhai mchezo huo kwani wanaona unazo changamoto nyingi.

Wapiga kura wanapaswa kuwa makini katika uchaguzi huu ili kukiwezesha Chaneta viongozi watakaosaidia kuuendeleza mchezo huo kimataifa. Kwa upande wa kitaifa, mchezo huo umeenea kwa kiasi fulani na Chaneta walijitahidi kuendesha mashindano pamoja na mafunzo ya uamuzi na ukocha katika mikoa tofauti tofauti.

Hata hivyo, tatizo liko kwa upande wa mchezo huo kimataifa kwani Tanzania imeshindwa kabisa kupenya licha ya huko nyuma kufikia hadi nafasi ya 13 kwa ubora wa viwango duniani.

Kwa sasa Tanzania haimo kabisa katika viwango hivyo na sababu kubwa ya Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA) kutoipanga ni Chaneta kushindwa kupeleka timu za taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa sababu ya ukata.

Ikumbukwe kuwa, moja ya majukumu ya viongozi ni kuweka mipango sawia ili kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali na hilo wagombea wengi hasa wale wa nafasi za juu wamekuwa wakijinadi kulitekeleza mara watakapoingia madarakani.

Hatutaki kuwaelekeza wapiga kura nani wamchague, au nani wasimchague, lakini wao ndiyo wanawajua vizuri viongozi wanaowafaa kwa maendeleo ya mchezo huo nchini. Miaka minne siyo midogo kwani wapiga kura wakifanya kosa la kuchagua viongozi ambao hawatawasaidia, basi wajue fika kuwa netiboli itaendelea kufanya vibaya kimataifa na hata kitaifa pia.

Netiboli ni moja ya michezo ambayo Tanzania iliwahi kutamba sana kimataifa kwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali na hata kutwaa taji la mabara. Mbali na kutwaa taji la mabara, pia wachezaji wa Tanzania walinunuliwa na klabu za ughaibuni kwa ajili ya kwenda kuwa wachezaji wa kulipwa.

Na hilo la kuwa katika viwango vya juu kiubora katika mchezo huo na kuwa na wachezaji wa kulipwa nje ya nchi, vyote hivyo vilitokea au kuwezekana kwa sababu tu ya nchi kufanya vizuri katika mchezo huo kimataifa.

Kwa hiyo tunapenda kuwaambia wapiga kura watumie vizuri demokrasia yao kwa kuwachagua viongozi watakaoiondoa netiboli katika shimo na kuiweka mahali pazuri kimataifa.