Wakazi Shinyanga changamkieni fursa

MOJA ya hoja muhimu zilizotolewa jana katika Jukwaa la Fursa za Biashara Mkoani Shinyanga, ni pamoja na kutoa changamoto kwa wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa zitakozotokana na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoani Tanga, ambapo bomba hilo litapitia mkoani humo.

Akitoa changamoto hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema hatua ya ujenzi wa bomba hilo kupitia mkoani humo, ni fursa ambayo wananchi wa Shinyanga hawanabudi kuichangamkia badala ya kuwaachia fursa hiyo wageni.

Alisema wananchi hao wa Shinyanga waandae vijana wenye ujuzi kwa ajili ya viwanda na hata vibarua pale bomba la mafuta litakapopita wakiwemo mama lishe wenye vifaa vya kutosha kwa kazi hiyo.

Waziri Mwakyembe aliwakumbusha kwamba mkoa huo uko jirani na nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Rwanda, Burunndi, Uganda na Kenya, hivyo wasipochangamka fursa hizo zitachukuliwa na wageni.

Tunapenda pia kuunga mkono mwaliko wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kwa kuwakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani humo katika madini, ardhi, kilimo na ufugaji.

Tayari mkoa huo umetenga ekari zaidi ya 22,000 kwa ajili ya miundombinu ya shughuli hizo. Alifafanua kwamba kutokana na mkoa wake kuwa na neema ya madini ya dhahabu na almasi, amekaribisha wawekezaji kwenda kufungua viwanda vya kuongezea thamani mazao hayo ya almasi na dhahabu kwa maana ya kuzalisha vito kama mikufu, vidani na kadhalika.

Sambamba na kuwekeza kwenye viwanda vya madini zipo fursa pia za kuwekeza kwenye viwanda vya nguo, nyama na ngozi na usindikaji wa mazao mbalimbali ya kilimo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inayolenga kujenga uchumi unaotegemea viwanda hivyo kupanua ajira na bidhaa za kuuza nje ya nchi kuongeza mapato ya serikali na wananchi kwa ujumla wake.

Inatia moyo kupata habari kwamba tayari mkoa huo una viwanda 81 vikiwemo vikubwa, vya kati na vidogo vingi kati yake ni vya kuchakata mazao ya kilimo na hivyo kutengeza soko kwa ajili ya malighafi ikiwa ni pamoja na pamba, alizeti, matunda, maharage, soya na pumba za mpunga.

Hiyo bila shaka ni fursa nzuri nyingimne kwa wakulima kwani wana soko la uhakika na hivyo walichangamkie wabadilike katika maisha yao kiuchumi. Hili linawezekana kwa kuzitumia sawia fusra hizo.Tuzitumie kwa umakini.