Mabasi ya abiria yakaguliwe ipasavyo

TUKIO la ajali ya kufa maji watu 12 na wengine kuokolewa baada ya gari walilokuwa wakisafi ria aina ya Toyota Hiace, kutumbukia Ziwa Victoria baada ya kugonga geti la kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, ni la kuhuzunisha na kusikitisha sana.

Tunapenda kuungana na Rais John Magufuli na Watanzania wengine wote kuzipa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ajali hiyo ambayo imeleta majonzi na simanzi si tu kwa wanafamilia na wakazi Mwanza, lakini kwa Watanzania wote.

Wenzetu waliofikwa na mauti wamepitia hali ngumu hadi kupoteza maisha na wale walionusurika kwa neema ya Mungu, ni tukio ambalo litaendelea kuwepo katika fikra zao siku zote.

Kwa mujibu wa mmoja wa mashuhuda Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) Mkoa wa Mwanza, Ferdinand Mshama, gari hilo lilitumbukia likiwa linatokea Buhongwa kupeleka abiria kivukoni, kabla ya dereva kusimamisha gari vizuri, breki zilifeli na hivyo kugonga geti la kivuko na kutumbukia ziwani.

Shuhuda huyu anakiri kuwa si mara ya kwanza kwa matukio ya magari yanayokwenda kivukoni, kufeli breki na kuingia majini na kwamba kati ya Septemba na Oktoba mwaka huu tayari yameshatokea matukio matano ya aina hiyo katika kivuko hicho.

Hii inamaanisha nini? Kuwa wahusika kwanza wa vyombo hivyo kwa maana ya mmiliki wa gari, dereva na kondakta hawawajibiki ipasavyo katika kuhakikisha usalama wa abiria au wateja wao na ndio maana yanatokea matukio haya.

Vilevile mamlaka husika wakiwemo wanaosimamia masuala ya usalama wa barabarani, hawajafanya kazi yao vizuri kuhakikisha wanadhibiti ama kuzuia magari yasiyokuwa katika hali nzuri kufanya shughuli ya kusafirisha abiria.

Imekuwa jambo la kawaida kuona magari yanayosafirisha abiria yakiwa katika hali mbaya, lakini unashangaa kuyaona yakiendelea kutoa huduma, ilihali wako wahusika wakiwemo askari wa usalama barabarani.

Kwa mtazamo wetu, kama Temesa yenyewe imekiri kwamba kwa kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba tayari yameshatokea matukio matano ya magari kufeli breki. Je, hatua gani zimechukuliwa kufanya ukaguzi wa vyombo hivyo kabla havijaingiza watu kwenye kivuko.

Matarajio yetu baada tu ya tukio la kwanza, ungekuwepo utaratibu mzuri wa magari na hili tukio la kusikitisha huenda lingeweza kuzuiliwa, ingawa upo usemi ajali haina kinga, lakini kuna nyingine zinatokana na uzembe mkubwa.

Ni imani yetu kuwa sasa serikali kupitia mamlaka zake husika, itaweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha matukio kama haya hayajitokezi tena, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa kina wa magari ili yale yenye matatizo yaache kutumika katika kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuelekea kivukoni na maeneo mengine ya mikoa yote nchini.