Wanasiasa Tanzania wajitafakari siasa za majirani

YAKO makubaliano ya wazi kabisa ambayo mataifa mengi yametia saini, makubaliano ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Makubaliano haya yamelenga kuwezesha migogoro na amani katika mataifa hayo kutokea kwa maridhiano ya wao kwa wao. Makubaliano ya kutokuingilia masuala ya nchi nyingine kama yalivyo katika makubaliano ya Montevideo ya wajibu wa nchi na haki ya mwaka 1933, yanatoa nia ya dhati ya dunia kuiweka kuwa eneo la usalama na amani.

Kuna namna nyingi ya kuingilia siasa za ndani za nchi nyingine na katika maingilio hayo, mara nyingi wanasiasa ndiyo wanaanza chokochoko na kuleta hisia zenye mkorogo kwa mataifa mengine.

Hatuna shaka kwamba makubaliano ya kimataifa kuhusu kutoingilia masuala ya nchi nyingine, ni sheria tosha ya kimataifa na inayofaa kuzingatiwa si tu na taifa na serikali za nchi mbalimbali bali pia na kila mmoja kama tutataka maisha katika jamii yetu kuwa sawasawa na yenye kuwa na maana.

Katika Vikao vya Bunge la 11 mwaka huu, wapinzani nchini wakati wakijadili kuridhia itifaki ya amani na usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia msemaji, Cecilia Paresso alisema iko haja ya nchi wanachama kujikita zaidi kutafuta suluhu ya kidiplomasia katika migogoro kuliko kutumia nguvu za kivita.

Pamoja na mambo mengi Kambi hiyo ya upinzani pia ilitaka kupitiwa kila mara kwa itifaki hiyo ili kuona mwenendo wa utekelezaji wake, ikiwa ni pamoja na kuachana na viashiria vya kulipua mawazo hasi na vurugu katika nchi husika na nchi nyingine za jirani.

Katika misingi ile ile ya kudumisha na kuimarisha hali ya amani, usalama na utulivu katika eneo la Afrika Mashariki, pamoja na kukuza ujirani mwema kwa nchi wanachama, iko haja kwa wanasiasa wengi katika nchi hizi ikiwamo Tanzania kujitafakari na kuachana na tabia za kufanya siasa katika nchi nyingine.

Kwani kimsingi itifaki hiyo ambayo pia maandiko yake yamezingatia sheria za kimataifa, imejikita zaidi katika kuwalinda wananchi dhidi ya uvunjaji wa sheria unaoweza pia kusababishwa na upandikizaji wa maneno ya chuki, hasira kwa visingizo mbalimbali ikiwamo urafiki.

Kwa kuwa wanaopitisha itifaki hizi ni wanasiasa na kwa kuwa wanasiasa ndiyo wanaovunja pia makubaliano tunawasihi wanasiasa nchini Tanzania kuwaacha Wakenya katika siasa zao za ndani bila wao kutia mkono kwa sababu mbalimbali ili mtangamano wa Afrika Mashariki uwe na maana ya kweli katika siasa.

Hakuna mtu ambaye atafurahia vurugu nyingine kubwa katika moja ya nchi za Afrika Mashariki na kwa kweli ni kazi yetu kuzuia kulipuka kwa hali hiyo kwa kutokuwa na upande katika migongano ya nchi nyingine.

Tunatoa rai na kusisitiza tena falsafa ya ujirani inaonesha vyema kabisa haja ya wanasiasa wetu wakaacha kuchokoa jicho la jirani huku wakiangalia namna bora ya kutatua migongano ndani na nje ya nchi wanachama na hivyo kuzuia mitafaruku inayoweza kuzusha ghasia.

Ndiyo kusema kama itifaki inavyotaka, yaani kuzuia vitendo vya kuharibu kwa jumla au sehemu ya utaifa, uasili, ubaguzi wa rangi au dini, basi wanasiasa hapa nchini waone wajibu wa kusimamia itifaki hiyo na kuiacha Kenya ifanye mambo yake.

Hata kama tutakuwa tunajaribu kujitetea katika hili, lakini kitendo cha kuingilia kati siasa za Kenya kunakofanywa na wanasiasa wa Tanzania wengine wakiwa wameshawahi kuwa watawala nchini ni kuleta wingu zito linaloweza kuvunja matumaini na amani ambayo tayari ipo kwa Afrika mashariki. Tuwe makini na tujitafakari. Mungu Ibariki Afrika Mashariki, Mungu Ibariki Afrika.