Umakini unatakiwa pambano la Yanga na Simba

WATANI wa jadi, Yanga na Simba wanacheza leo kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam katika moja ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara raundi ya nane.

Mechi za watani zimekuwa zikiwagusa watu wengi hata wale wa timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo pamoja na zingine hapa nchini. Yanga na Simba zinakutana wakati timu hizo zikilingana kwa kila moja kuwa na pointi 15, lakini Simba wako juu kwa sababu ya kuwa na uwiano mzuri wa mabao.

Kutokana na ushindano uliopo kati ya timu hizo kwa kipindi hiki katika ligi, bila shaka mchezo huo utavutia watazamaji wengi, kwani kila shabiki atakuwa akitegemea ushindi kwa timu yake.

Mbali na ushindi huo, pia kitendo cha mchezo huo kuchezewa kwenye Uwanja wa Uhuru, ambao ni mdogo ukilinganisha na ule wa Taifa, hilo nalo litafanya uwanja huo kujaa pomoni mapema hata kabla ya kuanza kwake.

Uwanja wa Uhuru unachukua watazamaji takribani 24,000 wakati ule wa Taifa wenyewe unabeba watazamaji 60,000 wote waliokaa katika viti. Mchezo wa timu hizo mbili umekuwa na matukio mbalimbali ndani na nje ya uwanja, hivyo umakini mkubwa unatakiwa leo wakati timu hizo zinapokutana kwa mara ya kwanza katika ligi msimu huu.

Kuanzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Huduma ya Kwanza (Msalaba Mwekundu), Polisi pamoja na Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wote wanatakiwa kuwa makini katika mchezo huu wa leo.

Watu wa huduma ya kwanza wanatakiwa kuwa wa kutosha na kuwa na vifaa kwani watu watakuwa wengi na kutakuwa na matukio mengi ya kuzimia au kuumia, hivyo waboreshe huduma zao.

Kwa upande huo wa Huduma ya Kwanza au Msalaba Mwekundu, mbali na huduma za hapo uwanjani, pia kunatakiwa kuwepo na magari ya kutosha ya wagonjwa na yenye huduma zilizokamilika, kwani lolote linaweza kutokea.

Kwa upande wa watu wa usalama wakiwemo polisi na FFU, wanatakiwa kuwa makini kulinda usalama badala ya kuingia uwanjani kuangalia mpira na kujisahau. Tumeona mechi za Ulaya watu wa usalama huwa hawana mpango kabisa na mchezo unapoendelea uwanjani na badala yake wamekuwa wakiwageukia watazamaji, eneo ambalo ndiyo huwa na matatizo na siyo sehemu ya kuchezea, ambako waamuzi wako.

Kwa upande wa waamuzi, nao watakiwa kuchezesha kwa umakini mkubwa mchezo huo kwa kuzingatia sheria 17 za soka na siyo kupendelea timu moja ili kufurahisha nafsi au watu fulani.

Waamuzi wakati fulani wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani kama watachezesha mchezo kwa upendeleo na kuziacha sheria 17 za soka zikikaa pembeni. Hilo hatulitarajii kwani uamuzi unachangia kwa kiasi kikubwa mchezo kuwa na utulivu na amani kama tu utachezeshwa kwa kufuata sheria zote bila upendeleo wowote.

Baadhi ya waamuzi wamekuwa wakichezesha mchezo kwa kufuata utashi wake na siyo kufuata sheria za soka, kwani kufanya hivyo kutaharibu kabisa mchezo huo na kutompata mshindi wa kweli.

Mwamuzi wa kati, Elly Sasii kwa kushirikiana na wasaidizi wake ni matarajio ya wengi kuwa, watachezesha mchezo huo wa Simba na Yanga kwa haki bila upendeleo ili tupate mshindi wa ukweli na kuondoa malalamiko. Tunawatakia kila la heri watani wa jadi, Yanga na Simba katika pambano la leo, ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa soka ndani na nje ya nchi