Urasimu uondolewe kiwanda cha mbolea kianze

TAIFA likiwa na mwelekeo wa kuwa ni taifa la uchumi wa kati kwa kutegemea sehemu kubwa ya pato lake katika viwanda, kuwapo kwa uwekezaji mkubwa katika kiwanda cha mbolea kitakachozalisha tani milioni 1.3 ndiyo suluhisho la mabadiliko tarajiwa katika kilimo ili kikidhi mahitaji ya viwanda.

Uwekezaji huo wa dola za Marekani bilioni 1.9 wa kuzalisha mbolea Kilwa mkoani Lindi, ndiyo uwekezaji mkubwa ambao unapaswa kuunganishwa na sekta nyingine za umma ili matokeo ya uzalishaji huo umnufaishe zaidi mkulima mdogo.

Kampuni ya Ferrostaal ya Ujerumani na Halfor Topsoe ya Denmark kwa kuleta uwekezaji huu kwa pamoja kwa kuanzisha Tanzania Mbolea Petrochemicals (TAMCO) ambapo mahitaji ya mbolea nchini yakielezwa kuwa zaidi ya tani 350,000 kwa mwaka, kimsingi serikali nayo ikiingia itawanufaisha zaidi wakulima wadogo wadogo nchini.

Ni dhahiri bila mkono wa dola, itakuwa ngumu uwekezaji huo kuwanufaisha wakulima hao ambao kimsingi wanahitaji unafuu wa bei kwenye bidhaa hiyo ili kuleta tija kwenye uzalishaji wa mazao.

Kutokana na mazingira ambayo huwapo ya kiuchumi na hasa katika utafuitaji wa faida, Serikali isipoingilia kati wakulima wakubwa watameza wakulima wadogo na hivyo mapinduzi ya kilimo hayatawezekana.

Kwa kuwa katika nyaraka zake kampuni hizo za mbolea zilisema kuwa asilimia 30 ya mbolea itakayozalishwa itauzwa hapa nchini ni vyema serikali ikalisimamia jambo hilo ili wanufaika wakubwa wa asilimia hiyo 30 wawe wakulima wadogo kwa kuhakikisha bei ya mlaji inamwezesha Mkulima mdogo kuwa sawa.

Sisi tunaamini kwamba kuwapo kwa kiwanda hicho kutasaidia kusukuma mbele matumizi ya mbolea ya chumvichumvi nchini ambayo kwa sasa bado yako chini ikilinganishwa na mahitaji halisi.

Ni kweli kuwa matumizi ni madogo kwani kama eneo linalolimwa mahindi nchini linakadiriwa kuwa hekta 4,086,555 makadirio ni kuhitaji jumla ya tani 612,983 za mbolea kwa mwaka, mazao mengine kama nafaka, miwa, tumbaku, kahawa na chai yanahitaji wastani wa tani 204,013 kwa mwaka; ndiyo kusema kiwango cha mbolea kinachotakiwa nchini kwa mwaka ni kikubwa, lakini kwa sababu ya bei kuwa juu mahitaji ya mbolea ya chumvi chumvi kwa mwaka ni kama tani 500,000.

Kwa kuwa tunaamini kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa wakulima wadogo wanaoshindwa kupata mbolea kwasababu ya bei ya mbolea kuwa juu, tunaiomba serikali kufanya kila linalowezekana kiwanda hicho kuanza uzalishaji mapema na kusimamia hiyo asilimia 30 kuwafikia wakulima hasa wale wadogo ambao ndiyo tegemeo la taifa.

Ni dhahiri mbolea itakayozalishwa italeta fursa kubwa kwa wakulima wadogo, kuwabadili katika kilimo chao kuzalisha zaidi kwa ajili ya kulisha viwanda mbalimbali vikiwemo vya mafuta, chakula na nguo.