Afrika ijifunze somo la Mugabe

RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe juzi alijiuzulu baada ya shinikizo la taasisi mbalimbali za kiraia na ushauri wa viongozi akiwemo Rais wa zamani wa Zambia, Keneth Kaunda.

Aliachia madaraka siku chache tangu Jeshi la nchi hiyo kutangaza kuwakamata watu 40 wanaounda mtandao wa G40 liliodai ni wahalifu wenye uhusiano wa karibu na mkewe, Grace.

Kuondoka kwa Rais Mugabe (93) kumefungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hiyo iliyopata uhuru wake mwaka 1980 kutoka kwa Uingereza iliyokuwa ikiitawala muda mrefu. Mugabe anaondoka akiwa ameacha rekodi ya kuwa kiongozi aliyeimarisha uhusiano mzuri na Tanzania tangu akipigania uhuru wa Zimbabwe.

Kwamba Mugabe ameondoka kabla ya kumaliza muda wake wa urais mwakani kwa shinikizo la jeshi na maandamano ya wananchi si jambo zuri hata kidogo kwa kiongozi huyo. Hata hivyo, kwa kuwa hatimaye kwa hiari yake amekubali kuachia madaraka baada ya kukataa mara kadhaa akihoji uhalali wa kuondolewa kwake, ni jambo linalostahili kumpongeza kwani limeepusha vurugu ambazo zingetokea.

Ni matumaini yetu kuwa, kuondoka kwake sasa kutawezesha wananchi wa Zimbabwe kupata fursa nzuri ya kurekebisha mapungufu ya utawala wake na kuendeleza mazuri yake pia.

Ni vyema Jeshi likasimamia haraka, taratibu za kuhakikisha Zimbabwe inapata uongozi wa kiraia utakaoendeleza pale alipoishia Komredi Mugabe ikiwemo uhusiano mwema na majirani.

Ni matumaini yetu aliyekuwa Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa anayetajwa kurithi urais huo kuelekea uchaguzi mwingine, atahakikisha Zimbabwe ni shwari na salama. Tunamtakia Mnangagwa kila la kheri tukiamini kwa kuwa msaidizi wa muda mrefu wa Rais Mugabe, anao uwezo mkubwa wa kuivusha Zimbabwe kutoka mgogoro huu.

Tunaziomba nchi nyingine za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC), majirani na hata jumuiya za kimataifa, kuiunga mkono Serikali mpya itakayoingia madarakani hivi karibuni. Hata hivyo, tunaamini yaliyotokea Zimbabwe yatabaki kuwa somo kwa wanasiasa mbalimbali na hata wananchi katika utekelezaji demokrasia.

Ni matarajio yetu kuwa baada ya kujiweka sawa, wananchi wa Zimbabwe watapata fursa nzuri ya kuendeleza nchi yao kiuchumi. Ingefaa basi wakaachwa kutafuta suluhisho la matatizo yao wenyewe tukiamini mambo haya yamewaachia somo kubwa kuhusu demokrasia