Kila la heri Kili Stars, Zanzibar Heroes Chalenji

MASHINDANO ya Kombe la Chalenji yanaanza kesho nchini Kenya, huku wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano hayo, Kilimanjaro Stars wanaanza kampeni zao kesho.

Wakati Kilimanjaro Stars wakianza mashindano hayo kwa kufungua dimba dhidi ya waalikwa Libya, wenzao wa Visiwani Zanzibar, yaani Zanzibar Heroes wataanza kampeni zao Jumanne, Desemba 5.

Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes zote ziko katika Kundi A na zimepangwa na timu za Kenya na Rwanda, ambazo sio za kuzibeza kwani ni timu nzuri na zenye viwango vya juu.

Kiujumla kundi hilo tunaweza kusema kuwa ni gumu kutokana na wapinzani wa Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kuwa na viwango vya juu kuliko Tanzania. Pamoja na Kilimanjaro Stars kuundwa na wachezaji kutoka Tanzania Bara tu na Zanzibar Heroes kuundwa na wale watokao kisiwani humo, lakini timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars huwa na wachezaji wengi wa Bara.

Na hata hao wachache wanaotoka Zanzibar na kuunda Taifa Stars wengi wao huchezea timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara. Kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa mwezi uliopita na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Tanzania iko katika nafasi ya 142 ikiporomoka kwa takribani nafasi sita.

Libya wako katika nafasi ya 77 wakipanda kwa nafasi 10 wakati Kenya wako katika nafasi ya 111 wakiporomoka kwa nafasi tisa, huku Rwanda wenyewe wakiwa katika nafasi ya 120 wakiporomoka kwa nafasi mbili tu.

Kutokana na viwango hivyo, Tanzania tuko chini ya timu zingine zote, ambazo ziko katika Kundi A, hivyo sio timu za kuzibeza kwani zinaonekana zina uwezo zaidi. Hata hivyo, pamoja na kuwa juu yetu, lakini wachezaji wa Taifa Stars na Zanzibar Heroes wasitishike na viwango hivyo na badala yake waoneshe uwezo wao kwa kuifunga timu moja hadi nyingine na kutwaa ubingwa.

Ndio ni kazi kubwa na ngumu lakini hakuna lisilowezekana katika soka endapo timu zetu hizo mbili zitapambana kwa nguvu. Huenda Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes zikachukuliwa kama timu zisizoweza kutwaa ubingwa kutokana na viwangi vyao pamoja na rekodi ya timu hizo katika mashindano hayo.

Kilimanjaro Stars imetwaa mara tatu tu taji hilo, 1974, 1994 na mwaka 2010 wakati Zanzibar wenyewe walitwaa taji hilo mara moja tu mwaka 1995. Wakati Uganda imetwaa mara 12 na Kenya ikilibeba taji hilo mara sita, hivyo Kilimanjaro Stars na Zanzibar zimetwaa mara chache na huenda zikachukuliwa kama timu dhaifu.

Timu hizo zinaweza kutumia udhaifu huo kufanya kweli na hatimaye kulitwaa taji hilo la Chalenji, ambalo ni mashindano makongwe zaidi barani Afrika ukilinganisha na mengine. Yote na yote, viwango na rekodi za kulitwaa taji hilo mara nyingi zote zimeshapita na sasa kinachoangaliwa timu gani itafanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu.

Wachezaji wa Kilimanjaro Stars pamoja na wale wa Zanzibar wasiwaogope kabisa wapinzani wao kwani wakicheza kwa kujituma watafanya vizuri na hata moja wapo kutwaa taji hilo. Tunazitakia kila la heri Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes katika mashindano hayo ya Kombe la Chalenji nchini Kenya mwaka huu.