Wababaishaji wajiondoe katika mradi wa DMDP

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema hataki kusikia wakandarasi wababaishaji kwenye utekelezaji wa Miradi ya Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Amewataka wahandisi na watendaji wa Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke ambazo zinatekeleza miradi hiyo kutokuwa na mjadala kuhusu suala la ubora wa barabara zao. Tunapenda kuungana na Waziri Jafo kusisitiza haja ya viongozi wa Serikali za Mitaa na Kuu kufanya kazi zao kwa ufanisi ili kuleta maendeleo.

Kwa muda mrefu watendaji wengi wamekuwa na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na hivyo kujikuta wakikwamisha au kuchelewesha miradi mingi ya maendeleo wanayotakiwa kuisimamia.

Hatuna lengo la kumnyooshea kidole mtendaji yeyote lakini tunadhani kauli ya Waziri Jafo ni ushahidi wa kutosha kuonesha kwa nini ni vizuri kila mwenye dhamana akawajibika nayo.

Kwamba mradi wa DMDP unagharimiwa kwa fedha nyingi si jambo la kujadili hivyo iko haja wahusika, watendaji wa Manispaa zote tatu, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wakandarasi husika, wakausimamia vyema.

Hatutarajii miradi huo wa barabara mbalimbali za Dar es Salaam utatekelezwa chini ya kiwango na kugeuka mashimo ndani ya mwaka mmoja bali zitadumu na kulipa thamani yake.

Mradi huo unaogharimu sh bilioni 660 unafaa kuwa kielelezo cha nia ya dhati ya wananchi kuwa tayari kujiletea maendeleo ya haraka kwa kusimamia vyema miradi wanayoletewa nchini.

Kama anavyosema Waziri Jafo, itakuwa ni aibu kubwa kwa Jiji la Dar es Salaam ambalo ndio kioo cha maendeleo ya nchi, kuharibu mradi kwa kujenga barabara zilizo chini ya kiwango.

Kama majiji mengine ya Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na miji ya Kigoma Ujiji, Mtwara Mikindani yamefanikiwa kujenga barabara nzuri katika Mradi wa Uendelezaji wa Miji Kimkakati (TSCP), Dar es Salaam na Manispaa zake zitashindwaje mradi wa DMDP.

Ni vyema wakati huu ambapo Serikali inahamia Dodoma, watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Manispaa zote tatu wakatumia fursa hiyo kuimarisha miundombinu kutokana na kupungua magari ili kuwa na miundombinu mizuri itakayodumu kwa muda mrefu ujao.

Tunaungana na Waziri Jafo kukemea watendaji wote wazembe, wasio na uwezo, uadilifu na pia wasiojituma tukiamini kuwa, watendaji wabovu kama hao wataishia kuharibu miradi kama hiyo.

Ifike wakati kwa wale wanaojipima na kuona hawatoshi kusimamia mradi kama huo na hata mingine inayotekelezwa na Serikali, wajiondoe kabla ya hatua anazosema Jafo kuchukuliwa.