TFF iongeze umakini Ligi Daraja la Kwanza

SHIRIKISHO la Soka Tanzania linatakiwa kuwa makini zaidi katika kipindi hiki cha mwisho cha Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Tunaweza kusema kuwa sasa ligi hiyo imefi kia hatua ya lala salama wakati ikielekea mwishoni kabisa katika mbio za kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao. Ligi Daraja la Kwanza ni muhimu sana katika maendeleo ya soka hapa nchini na ndiyo maana tunawataka viongozi wa TFF kuwa makini katika kindi hiki.

Ubora wa timu zinazoshiriki ligi hiyo ndiyo msingi imara wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho, ambazo hutoa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Jumla ya timu 24 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika kundi, ambapo kila kundi lina timu nane na timu mbili za kwanza ndizo zitakazopanda daraja na kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Mwendo wa ligi hiyo daraja la kwanza unajulikana kwani tumeona timu zikicheza na kupata matokeo yasiyo ya haki, kwani baadhi zimekuwa zikibebwa. Ndio maana tunasema kuwa TFF hasi Bodi ya Ligi iwe makini zaidi katika kipindi hiki kwani ndicho hasa rafu huchezwa na kusababisha kupatikana kwa washindi wasiohalali.

Hapa kuna vitu viwili, kimoja ni timu kupambana kucheza Ligi Kuu Tanzania, ambapo zinatakiwa jumla ya timu sita, kila kundi linatoa timu mbili za kwanza. Jambo la pili ni zile timu zinazopambana kutoshuka daraja, ambazo nazo zinapigania kuendelea kubaki katika Ligi Daraja la Kwanza ili mwakani zisianzie Daraja la Pili.

Katika mapambano hayo ya kupanda daraja na yale ya kubaki katika ligi hiyo hapo ndipo tatizo linatokea kwani baadhi ya timu, hasa zile ambazo hazina nafasi kwani zinaweza kufanya mchezo mchafu.

TFF isipokuwa makini tunaweza kupata timu mbovu zitakazopanda, ambazo hazitaleta upinzani katika ligi hiyo ambayo msimu ujayo itashirikisha jumla ya timu 20. Timu mbili ndizo zitakazoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara na kucheza Daraja la Kwanza, hivyo timu nyingi sasa zinanafasi ya kucheza Ligi Kuu.

Hivi sasa kila timu imebakisha michezo miwili au mmoja mkononi ili kumaliza ligi hiyo na kujua nini imevuna. Hivyo ni vyema basi timu zote zikahakikisha zinacheza kwa nguvu kwa nia ya kupata ushindi na kusiwe na upangaji wa matokeo wa aina yoyote kwa nia ya kuzibeba baadhi ya timu na kuzikandamiza nyingine.

Haya mambo ya kubebana ndiyo yatasababisha zipande timu, ambazo hazina uwezo na matokeo yake zinakuwa dhaifu katika Ligi Kuu. Tumelazimika kutoa angalizo kulingana na jinsi msimamo wa ligi ulivyo, ambao unatoa mwanya wa baadhi ya timu, ambazo hazina uhakika wa kushika nafasi za juu, au haziwezi kushuka daraja kuamua kupanga matokeo ili kujipatia.

Upangaji matokeo siyo lazima uwe kwa timu na timu, bali hata viongozi wakiamua kuwarubuni baadhi ya waamuzi wapendelee timu yao nalo si jambo la busara hata kidogo. Tunatoa tahadhari kwamba michezo hii ya mwisho kuna haja ya klabu zote zikazidisha uadilifu ili imalizike bila kupanga matokeo kwa aina yoyote.

Tunasema timu zote zinazoshiriki ligi hiyo zihakikishe haziingii uwanjani na matokeo yao mikononi, kwani mshindi halali ni yule anayepatikana uwanjani na si vinginevyo. Ni jambo zuri kama timu hata inaposhuka daraja inatakiwa inapambambana hadi dakika za mwisho bila kujali nafasi yao. Waamuzi nao wanatakiwa kutenda haki, kwani nao ndiyo tatizo kubwa na kama wakifanya vizuri basi washindi halali watapatikana