EAC ijipange kueneza Kiswahili duniani

NCHI sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zina kila sababu ya kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili, ambayo karibu kila mwananchi katika nchi hizo ama anaitumia moja kwa moja ama anaijua kuwa ipo na ni muhimu katika mawasiliano baina yao kuliko lugha nyingine yoyote.

Wanachama wa EAC ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Nchi hizo zina makabila mbalimbali kwa mfano Tanzania ina zaidi ya makabila 120, Kenya makabila zaidi ya 40 na hali kadhalika nchi nyingine wanachama zilizobakia zina makabila yao pia.

Licha ya ukweli kwamba lugha hiyo ndiyo lugha pekee kwa Tanzania iliyofanikiwa kuunganisha makabila yote bila kuhitaji lugha nyingine kwa yeyote anayetaka kulihutubia taifa la Tanzania, ni ukweli pia kwamba lugha hiyo ya Kiswahili uimara wake unatokana pia na ukweli kwamba haihusishwi na kabila lolote.

Mtaalumu mmoja wa lugha hiyo ya Kiswahili, Dk Rajabu Chipila katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni alibainisha wazi kwamba sifa hiyo ya pekee ya kutohusishwa na kabila lolote lile Afrika na hata duniani ndiyo imekuwa ni kuchocheo cha aina yake kwa lugha hiyo kupendwa na watu wengi kujifunza na kuielewa.

Tuna kila sababu kama nchi wanachama wa EAC kuisambaza kwa nguvu zote lugha hiyo ndani ya nchi zetu lakini pia kuipeleka kwa nchi nyingine za Afrika na dunia kwa ujumla wake kwa sababu kubwa moja, EAC ndiko nyumbani kwa lugha hiyo na wataalamu waliobobea lugha hiyo kwa maana ya kuiwezesha kusambaa nje ya bara hili, ni watu wa EAC.

Ni jambo la kujivunia pia kwamba lugha hii ya Afrika Mashariki tayari imeshaanza kutumika kufundishia masomo ya elimu ya msingi nchini Tanzania, lakini pia imeshaanza kutumika pia nchini Rwanda katika shule zake mbalimbali.

Sambamba na hatua hiyo lugha hiyo pia inafundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani. Vyuo hivyo ni pamoja na vya Marekani, Ujerumani, Uingereza, Japan na Korea Kusini.

Sambamba na kufundishwa vyuo vikuu, lugha hiyo pia hutumika katika vyombo mbalimbali vya habari katika mataifa makubwa kama Ujerumani, Uingereza, Japan, Ufaransa na Urusi. Hakuna ubishi kwamba Kiswahili ni fahari yetu ya Afrika.

Tunapenda kutoa mwito kwa nchi wanachama wa EAC kuungana kwa pamoja katika kukuza lugha yetu ya Kiswahili ndani na nje ya nchi zetu, tukilenga pia kupanua ajira kwa wananchi wetu kupitia ufundishaji wa lugha hiyo adhimu ya Afrika katika nchi mbalimbali duniani.

Tusiwe watazamaji katika ajira zinazotokana na lugha ya Kiswahili, bali tuwe hasa watendaji wa kutolewa mfano katika utekelezaji wa ufundishaji na usambazaji wa lugha ya Kiswahili. Mwisho