Jamii iwe tayari kukomesha rushwa

 ILI Serikali iweze kufanikiwa katika dhamira yake ya kukomesha rushwa nchini kwa kuhakikisha mtu anapata kazi au kupanda cheo kwa sifa wala si kwa kutoa rushwa ya fedha au ngono, ni lazima jamii iwe tayari kubeba dhana hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, Selemani Jafo, rushwa ni tatizo katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za afya na elimu.

Waziri Jafo anasema kumekuwa hakuna haki, watu wamekuwa wakinyanyaswa mara wanapotakiwa kupanda vyeo au kupata kazi wakitakiwa watoe rushwa ya fedha na kwa wanawake, wakilazimika kukubali kufanya ngono ili wapate kazi au msaada mwingine muhimu kutoka kwa watoa huduma.

Jafo alisema hayo juzi Dodoma wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kupiga vita rushwa kuanzia shuleni na kampeni ya kupiga vita mimba za utotoni.

Jamii inaelewa fika kwamba tatizo hili ni kubwa na limekuwa likitafuna wanyonge kwa muda mrefu.

Inaeleweka fika kwamba ni mazoea ambayo yamewanyima haki wenye kustahili na kuwapa faraja watoa rushwa kupata kile ambacho hawakuwa na uhalali nacho.

Tunampongeza Waziri Jafo kwa kulisemea hili na serikali kwa jumla zikiwemo taasisi zinazojihusisha na kuzuia rushwa ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini kama alivyonukuliwa akisema, bado juhudi za kupambana na rushwa nchini zinahitajika kwa jamii nzima kushiriki kikamilifu.

Tunaendelea kuyahimiza pia mashirika ya kitaifa na kimataifa, likiwemo Shirika la Creative Plan ambalo kwa sasa limeanzisha kampeni ya kuelimisha wanafunzi, likilenga nchi nzima kupinga vitendo vya rushwa kupitia klabu zao zilizoundwa katika kila mkoa kwani rushwa ni adui wa haki.

Jitihada hizi zimeanza kuzaa matunda taratibu ndio maana kupitia ripoti ya taasisi ya Transparency International, Tanzania imepanda kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 116 mwaka 2016 hadi nafasi ya 104 mwaka jana, huku ikipata pointi 36 mwaka jana kutoka pointi 32 za mwaka juzi.

Pia Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa Afrika mashariki huku ikiongozwa na Rwanda ambao ilishika nafasi ya 48 kwa mwaka jana huku ikiwa na pointi 55.

Tanzania iko juu ya jirani zetu, kama Kenya iliyoshika nafasi ya 143 wakati Uganda ikishika nafasi ya 151, na hivyo kuifanya Kenya kuwa kwenye nafasi ya tatu Afrika Mashariki huku Uganda ikishika nafasi ya nne.

Burundi inashika nafasi ya 157 na Sudan Kusini ikawa katika nafasi ya 179 kati ya nchi 180. Bado tunaamini, rushwa iko ndani ya jamii na kama itakuwa tayari kushiriki katika kupiga vita hii pana, kampeni hizi zitatupeleka katika kipindi kijacho kuwa katika nafasi nzuri zaidi kwenye ripoti ya viwango hivi vya rushwa kwenye mataifa 180 duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo, mwaka jana, nchi ya New Zealand na Denmark ndizo zilizoongoza kwa kuwa mataifa yasiyokuwa na hali ya rushwa.

New Zealand ilipata pointi 89 na kushika nafasi ya kwanza wakati Denmark ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 88. Kama nchi hizi mbili zimeweza, kwa nini Tanzania ishindwe kufikia lengo lake hilo? Kwa pamoja tunaweza.