Wasanii jifunzeni kutoka kwa nyota wazoefu kutoka Nigeria

HiVi majuzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpokea ofisini kwake msanii mahiri wa filamu kutoka nchini Nigeria, Mike Ezuruonye.

Msanii huyo aliwasili nchini wiki iliyopita kwa ziara ya siku 10 ambapo kwa sasa amebakiza takribani siku tano ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kutangaza Afrika kwa njia ya sanaa ya uigizaji.

Uwepo wake umeratibiwa na kampuni ya Burudani na Ubunifu, EPD, inayomilikiwa na mwigizaji wa muda mrefu nchini Halima Yahaya, maarufu kama Davina.

Binafsi mbali na kumpongeza mwanadada huyo kwa jitihada zake hizo ningependa kuwasihi wasanii wa hapa nchini kutumia ujio wa wasanii wakubwa kama hao kujiendeleza.

Ikumbukwe kuwa msanii huyo sio wa kwanza kufika hapa nchini kwa kuwa wapo wengine kama Ramsey na Omotola ambao waliwahi kufika hapa nchini kikazi.

Ramsey aliletwa na aliyekuwa msanii mahiri wa filamu za Bongo Movies, Marehemu Steven Kanumba huku Omotola msanii mahiri mwanamke, aliletwa na mwigizaji Wema Sepetu.

Jithada kama hizo ni nzuri kwa kuwa zinaonesha ni kwa kiasi gani wasanii wa Nigeria wanaipenda na kuikubali Tanzania na kuja kufanya kazi na wasanii wa hapa ila binafsi ninaona kuwa ni kama vile wasanii wa hapa hawatumii fursa kama hizo kujiongeza.

Ni wazi kuwa sanaa ya Nigeria imekua na inapendwa zaidi barani Afrika, huku wasanii wake wakiwa wanajipatia fedha nyingi kupitia sanaa, ndivyo hivyo kwa filamu za Bongo Movie kwa kuwa zinatumia lugha ya Kiswahili, lugha inayotumiwa zaidi Afrika Mashariki na Kati ni wazi kuwa nazo zina soko.

Sasa wasanii wa Nigeria wameliona soko hilo na ndio maana wameona kuwa kuna haja ya kujihusisha zaidi na sanaa za Tanzania kwa kuwa ni mwanya mkubwa wa kuliingia soko la Afrika Mashariki na Kati.

Sasa kwa ujio wao wa hapa nchini je ni kwa kiasi gani wasanii wa Tanzania wanajipanga katika kuwatumia wasanii hao wa Nigeria kujikita katika kufanya kazi Nigeria.

Waziri Nape amekuwa akiweka wazi nia yake ya kuendeleza sanaa ya filamu hapa nchini kwa kuwa anaamini kuwa ni njia mojawapo ya kuitangaza nchi ya Tanzania kwa njia ya filamu au aina yoyote ya sanaa.

Sasa kwa wasani wa hapa nchini ni vema mkajipanga na nyie kujiongeza kwa kuangalia uwezekano wa kujitangaza zaidi na kufanya filamu na wasanii wa Nigeria ili kujitangaza kwenye soko lao hilo.

Kama wasanii wa Nigeria wamefanikiwa kupata mafanikio kwao na mpaka sasa wameona soko kwenye nchi za Arika Mashariki na Kati, iweje wa hapa nchini washindwe kulitumia soko la Afrika Mashariki na Kati huku kwao wana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo.

Filamu inaweza kuziunganisha nchi za bara la Afrika kwa kuwa ni njia mahiri ya kuunganisha tamaduni za makabila na mataifa mbalimbali.

Waigizaji wa hapa nchini watumie ukaribu wanaouonesha wasanii wa Nigeria katika kujitengeneza mazingira ya wao kufanya kazi za sanaa Nigeria pia ili soko la filamu za Tanzania lifike Nigeria pia.