Barabara ya Hospitali ya Vijibweni itupiwe macho

PAMOJA na jitihada za serikali za kuimarisha miundombinu, lakini bado kuna changamoto za miundombinu hasa ya barabara katika maeneo mengi nchini.

Tatizo hili kwa wananchi wanaweza wakaliita ni kero kwa kuwa ni moja ya huduma muhimu wanazostahili kupata, lakini unakuta wanachokipata ni tofauti na matarajio yao.

Nimelazimika kuandika haya baada ya kuona wananchi wengi, hasa wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani wanaoitumia Hospitali ya Vijibweni kulalamikia ubovu wa barabara ya kuingia hospitali hiyo ukitokea eneo la Magengeni.

Hospitali ya Vijibweni ni moja ya hospitali kubwa katika Jiji la Dar es Salaam ambazo zinatoa huduma nyingi kwa wananchi ikiwemo upasuaji.

Hospitali hii pamoja na kutoa huduma hizo nzuri, lakini bado kuna changamoto inayowakabili wananchi ya kufika katika eneo hilo kutokana na ubovu wa barabara.

Mara nyingi wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakiiomba serikali kusikia kilio chao na kuwajengea barabara ya kiwango cha lami kuingia katika hospitali hiyo, lakini hadi sasa bado hali ni kama kawaida na barabara hiyo imekuwa ikiongezeka kuwa na mashimo.

Karibu kila mwaka barabara hiyo imekuwa ikichimbwa na kujazwa kifusi na mvua zinaponyesha mara moja huharibika na kubaki makorongo na hivyo kuwa kero, adhabu na mateso kwa wagonjwa na wananchi wanaoitumia barabara hiyo.

Kwa mfano, eneo linaloitwa kwa Mwarabu kabla hata mvua za masika hazijaanza kuchanganya, lakini tayari eneo hilo katika barabara hiyo inayokwenda Hospitali linapitika kwa shida kutokana na kujaa maji na hivyo kusababisha mashimo.

Maeneo kama hayo na kero kama hizo tunaamini uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni kwa kushirikiana na Mbunge wa Kigamboni, Meya na Madiwani wanaweza kuyafanyia kazi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Tusisubiri mpaka barabara ikashindwa kupitika kabisa ndipo muanze kuchukua hatua, tunajua uwezo mnao wa kutatua na kumaliza kero hii kwa wananchi na wakazi wa Kigamboni pamoja na wa maeneo jirani ambao wanaitumia hospitali hiyo.

Tunaamini kwa mwaka huu wa fedha, mtakaa na kujipanga kwa ajili ya barabara hii na kitu kikubwa kitafanyika na kuitupia macho barabara hiyo ambayo imekuwa ikitumika sana kutokana na huduma zinazotolewa.

Hospitali hiyo ikijengwa barabara kwa kiwango cha lami, naamini hata kero za mara kwa mara na malalamiko ya wananchi kuhusu mashimo na maji kutuama katika baadhi ya maeneo itakwisha.

Tunaelewa kwamba keki ni ndogo na wengi wanastahili kumegewa kidogo kidogo, lakini ni vyema pia wakaangaliwa wale ambao wanakaribia kufa kwa njaa ndo wakamegewa keki hiyo kwa haraka zaidi.

Kwa kuwa hospitali hiyo inahudumia wananchi wengi, hebu fikiria mjamzito anatoka akitikiswa mpaka anafikishwa hospitali au mgonjwa ametoka kufanyiwa upasuaji anatoka akitikiswa mpaka akakutane na barabara ya lami.

Siyo kwamba maeneo mengine hayatokei hayo, ila kwa kuwa hapa ni mjini na ndiyo karibu zaidi na mahali huduma zinatolewa lazima mipango yake iwe tofauti.

Hata katika familia tunajua yule aliye karibu na wazazi ndiyo huwa anafaidi. Hivyo tunaomba barabara hiyo itupiwe macho. Kwa kuwa Serikali yetu ni sikivu, tunaamini kero hii itafanyiwa kazi ili kuhakikisha wananchi wa Kigamboni wanapata suluhisho la barabara hiyo.

Lakini pia wakati mkisubiri suluhu ya muda mrefu ni vyema kwa sasa mkaangalia namna ya kuitengeneza barabara hiyo hata kama ni kwa kiwango cha changarawe na kufukia mashimo ili iweze kupitika kwa urahisi kabla mvua hazijaanza.