Watanzania wanawajibika kuisaidia TFDA katika hili

HIVI karibuni Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ilifanikiwa kukamata vyakula ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kukosa ubora unaotakiwa kisheria.

Mamlaka hiyo kupitia msako wake ilioufanya wilayani Kahama, ilifanikiwa kukamata jumla ya tani 2.2 za mchele, tani 5.9 za unga wa sembe na tani 9.2 za chumvi.

Mafanikio ya mamlaka hiyo yalitokana na msako wake wa ghafla katika majengo 274 ambayo kati yake 274 yalikuwa ni ya vyakula, maghala 11, magari na pikipiki.

Pamoja na operesheni hiyo, pia mamlaka hiyo siku mbili zilizopita ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kushikilia kwake, takribani tani 100 za mchele kutoka Pakistan ambazo hadi sasa hazijathibitika kama ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Ukweli ni kwamba, kwa kiasi hicho cha vyakula vilivyokamatwa kupitia msako huo, inaonesha bado kuna tatizo kubwa la uingizaji nchini wa bidhaa zisizo na ubora ikiwemo vyakula.

Hakuna asiyefahamu madhara ya kutumia vyakula visivyo na ubora kwa afya ya binadamu yeyote ikiwemo magonjwa makubwa kama ya ini na hata vifo.

Kwa hali hiyo, ni wakati sasa wa Watanzania kuamka na kuacha kuwakumbatia wafanyabiashara wasio waaminifu wenye tama ya kujinufaisha bila kujali madhara yatokanayo na biashara zao.

Vita hii dhidi ya bidhaa feki na vyakula visivyo na ubora vinavyoendelea kuingizwa nchini kwa njia za panya, ni ya Watanzania wote vikiwemo vyombo vingine vya usalama na si TFDA pekee.

Mfano mzuri ni kwa operesheni iliyofanyika Kahama iliyoshirikisha uongozi wa wilaya hiyo na kufanikiwa kukamata shehena hiyo ya vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu.

Endapo ushirikiano huo, utaoneshwa na maeneo mengine hasa yale ya mipakani na yale yenye njia maarufu za panya, ni wazi kuwa mapambano dhidi ya tatizo hilo yatafanikiwa.

Pamoja na hayo, ni wakati sasa Watanzania waelimishwe juu ya umuhimu wa kukagua bidhaa yoyote wanayoinunua kabla ya matumizi, kwani kwa kufanya hivyo wataweza kunusurika kununua bidhaa zilizokwisha muda wake na hata kugundua bidhaa zisizo salama.

Aidha, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mamlaka ya TFDA katika kushughulikia tatizo la bidhaa feki, ni vyema mamlaka hiyo ikabuni mbinu mpya za kudhibiti uingizwaji kiholela wa bidhaa nchini kutokana na ukweli kuwa wafanyabiashara wengi wasiowaaminifu nao huja na mbinu mpya kila kukicha.

Viongozi wengi walishakemea suala la Tanzania kugeuzwa shamba la bibi kwa maana ya kila mfanyabiashara asiyemwanifu kuitumia nchi hiyo na kuingiza bidhaa zake feki hali ambayo ki ukweli ni hatari kwa afya za wananchi endapo isipodhibitiwa.

Jitihada za kupambana na tatizo hilo, hazina budi kupewa kipaumbele kama ilivyokuwa kwa vita dhidi ya dawa za kulevya na viroba kutokana na madhara yake kwa binadamu, kwani hata matumizi ya vyakula visivyofaa kwa binadamu nayo ni hatari kwa usalama wa wawatumiaji.

Kwa ujumla, Tanzania imebarikiwa kuwa na vyombo mbalimbali vya udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini pamoja na TFDA, lakini pia lipo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Jeshi la Polisi, vyombo vyote hivyo, vikifanya kazi kwa pamoja na kushirikisha wananchi kikamilifu vitafanikiwa katika vita.