Tukiyaita majanga tusilaumu yakija

HIKI ni kipindi cha mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

Kipindi cha mvua baada ya kiangazi cha muda mrefu kilichoathiri uzalishaji wa mazao katika maeneo mengi nchini. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inazidi kusisitiza wananchi katika maeneo yao, kuchukua tahadhari kutokana na athari zozote zinazoweza kujitokeza. Tusipuuze.

Gazeti hili toleo la jana liliripoti mintarafu zaidi ya watu 1,800 katika vijiji kadhaa wilayani Ulanga katika Mkoa wa Morogoro, kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kuzingirwa na maji ya mafuriko yaliyotokana na mvua.

Jijini Dar es Salaam, mvua zimeripotiwa kusababisha adha kutokana na barabara kujaa maji zinaponyesha, hivyo kuzua kero ya usafiri na maeneo kadhaa nyumba kuingiwa maji.

Hali iko hivyo kwa maeneo mbalimbali nchini. Kwa Jiji LA Dar es Salaam hali hii imekuwa ada; kwamba hata mvua kidogo husababisha kero hadi katika huduma za usafiri kutokana na msongamano unaosababishwa na maji kujaa barabarani na kusababisha madimbwi.

Hii pamoja na mambo mengine, inachangiwa pia na kuwapo kwa miundombinu mibovu na inayojengwa chini ya kiwango na wakandarasi wasio waaminifu.

Ndio maana kwa nyakati tofauti, Rais John Magufuli na wasaidizi wake akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wamekuwa wakikemea vikali wakandarasi wanaofanya ujenzi wa barabarani chini ya kiwango.

Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba sasa Watanzania hatuihitaji mvua, la hasha tunaitaka, lakini tuzingatie kuwa usipoziba ufa, utajenga ukuta maana mchuma janga, hula na wa kwao.

Kwa msingi huo, kila mmoja kadiri ya uwezo wake, achukue tahadhari za kujilinda yeye mwenyewe, pamoja na jamii inayomzunguka tangu ngazi ya mtu binafsi, familia hadi taifa.

Ulinzi si lazima uwe ule tu, wa mipaka ya nchi au dhidi ya wahalifu wa makosa ya jinai, bali pia ule wa kuepuka majanga kama madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha kiangazi kikali au mvua zisizo na mpango, au za kiasi cha kupindukia.

Ingawa kwa kiasi kikubwa mafuriko ni moja ya majanga ya asili, mara nyingi pia madhara yake huchochewa na kazi za kibinadamu ukiwamo ujenzi na makazi holela, hasa maeneo hatarishi ya mabondeni.

Kimsingi, tunapaswa kujiepusha na majanga kama haya ambayo kwa kupuuza tahadhari, tutakuwa tunayaita wenyewe hivyo yakija, tusilaumiane wala kuilaumu Serikali kwa makosa yetu wenyewe.

Watanzania hatuna budi kukumbuka madhara ya mvua yaliyotukumba katika miaka ya hivi karibuni, huku wengine tukiathirika kutokana na ukaidi wa kupuuza maelekezo ya viongozi na wataalamu wa hali ya hewa.

Tukumbuke kipindi kama hiki cha mvua, ni rafiki kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hasa kama hakuna nidhamu na umakini katika usafi na matumizi sahihi ya maji, vyakula na mazingira.

Iwe ni aibu sasa kwa kila Mtanzania kujenga katika maeneo ya mabonde na mikondo ya maji. Kujenga na kuishi huko, ni kuita au kuchuma majanga maana mchuma janga, hula na wa kwao.

Kufanya hivyo ni kuchezea sharubu za simba. Kila mmoja aone na kujua kuwa ni aibu na hatari kugeuza mitaro ya maji kuwa sehemu za kutupa takataka, au kuruhusu takamwili zilizo katika vyoo vyetu nyumbani (kutapisha vyoo).