Ni wakati wa viongozi wa dini kujiangalia upya

KATIKA siku za karibuni kumekuwepo na malumbano yasiyokuwa na tija ambayo yamekuwa yakifanywa na wale waliopewa heshima ya kuwaongoza wengine katika nyumba za ibada.

Baadhi ya viongozi hao wa dini wamekuwa wakitumia sehemu za ibada kama za mashambulizi kwa watu wengine, hali inayoleta mshangao kwa wengine kama sehemu hiyo imegeuka kama ni uwanja wa siasa au la.

Lakini pia kumekuwa na tabia kwa viongozi hao wa dini kuacha kumaliza tofauti walizo nazo ndani ya taasisi zao na kuzitoa nje ambako wengine hawastahili kuzisikia. Tumeshuhudia viongozi wakitumia maeneo ya ibada katika kutoa mipasho ama kufanya siasa, jambo ambalo sio sahihi.

Kwa kutumia eneo hilo la ibada viongozi hao huzungumza kile ambacho wanafikiri ni sahihi, kwa kutoa mashambulizi kwa watu ambao wamekuwa wakitofautiana. Hilo sio sahihi kwa sababu kwenye nyumba za ibada kazi yake ni kumwomba na kumwabudu Mungu.

Pia wapo viongozi wengine ambao wamekuwa wakilumbana hadharani kwenye vyombo vya habari na hata wawapo kwenye maeneo yao ya ibada chanzo kikiwa ni kugombania uongozi, kutuhumiana kuhusu fedha ama kujibizana kwa lengo la kuaibishana.

Katika siku za karibuni kanisa moja lilikuwa kwenye mgogoro mkubwa wa kiuongozi hata kufikishana mahakamani baada ya kushitakiana.

Kutokana na kutokuelewana huko kulisababisha siku moja askari wa kutuliza ghasia na magari yenye maji ya kuwasha kuweka ulinzi chini ya kanisa hilo baada ya kiongozi mmoja alipotaka kutoa mahubiri yake kwa waumini.

Hilo kwangu lilinishangaza na kujiuliza kuwa, kanisa la leo linaelekea wapi? Hivi ni kweli viongozi hao walishindwa kupatana ndani ya kanisa na kuwafanya watu wengine wasiohusika kupata faida kwa kile walichokuwa wakituhumiana?

Baada ya kuripotiwa sana kwenye vyombo vya habari hatimaye mmoja wa viongozi hao aliamua kuondoa kesi aliyoifungua ili jambo hilo liishie ndani ya kanisa.

Japo alifanya jambo jema kuondoa kesi hiyo mahakamani ilikuwa tayari kanisa limeshadhalilishwa kwa kuwa mambo ya kiimani yanapaswa kumalizwa kiimani.

Si kwa upande wa kanisa tu hata kwa upande wa dini ya Kiislamu tumeona baadhi ya viongozi wa dini hiyo wakitofautiana na wengine hadi kupelekana mahakamani kutokana na kushindwa kuafikiana.

Hali hii haijengi picha nzuri kwa watu wanaotutegemea kwa kuwa sote tunafahamu kwamba, dini au viongozi wa dini ni kimbilio la wengi au ni sehemu ambayo watu wenye imani zao wameweka tumaini kubwa.

Hivyo wanapokuwa sehemu ya mifarakano au wanasababisha mifarakano wanashindwa kueleweka. Viongozi wa dini wafike mahali wamtumikie Mungu aliyewaita katika huduma yao hiyo na siyo vinginevyo, kwani kwa kutumia nyumba za ibada kuhubiri siasa ama mambo binafsi ni kwenda tofauti na neno la Mungu.

Sasa viongozi wa dini wafikie mahali wakatenganishe mambo ya Mungu na binafsi, ushauri kwa viongozi hao ni kwamba, ifike mahali wamtumikie Mungu aliyewaita kwa kujiepusha na malumbano yasiyo na tija ambayo hayana faida kwa watu wengine.

Na kama wameshindwa kuwa kwenye nyumba za ibada ni vema wakajiondoa na kujiingiza kwenye siasa ili wajulikane wamesimamia wapi.

Kama ni kutofautiana wanatakiwa wazimalize tofauti hizo ndani ya nyumba zao za ibada, haina faida kutunishiana misuli katika mambo hayo ya kiimani.

Au kwa wale ambao wamekuwa vipaza sauti vya kuwakosoa wengine kwenye nyumba za ibada ifike mahali waache tabia hiyo, kwani inawavunjia heshima kubwa.

Kwa kiongozi wa dini kutamka hadharani kuwa anaruhusu mapepo yamwingie mtu mwingine sio sahihi, kwani Mungu anataka waliokosea warejeshwe kwa upendo.

Kazi ya viongozi wa dini ni kuwaelekeza watu kuelekea kwenye njia inayofaa, kuwaongoza katika maadili mema, kuwaonya pale wanapokosea kwa kutumia maandiko pamoja na kuwafundisha neno la Mungu.