Ubomoaji wa mabondeni ufanyike haraka

IMEKUWA kama mazoea kwa watu wanaoishi katika maeneo hatarishi na mabondeni jijini Dar es Salaam, kuondolewa kipindi cha mvua na kurejea pale mvua zinapoisha.

Hali hii imekuwa ikisababisha maafa na vifo kwa baadhi ya watu katika vipindi vya mvua. Mbali na hivyo, pia hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara kwa serikali.

Hasara hiyo hutokea pale maafa yanapoonekana kwa baadhi ya watu mfano uokoaji, dawa na vyakula kwa waathirika. Mvua zilizonyesha juzi jijini Dar es Salaam, pia zilisababisha uharibifu wa mali na vifo kutokana na mafuriko.

Kutokana na hali hiyo, juzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alifanya ziara ya kuangalia athari na madhara ya watu walioathiriwa na mvua hizo.

Katika ziara hiyo, Makonda aliagiza kubomolewa kwa nyumba 36, ambazo zipo kwenye maeneo hatarishi ya mabondeni ikiwemo Bonde la Mto Msimbazi.

Watu hao inasemekana wengi wao walishalipwa na walishapewa viwanja katika eneo la Mabwepande, lakini bado wamekaidi na kurudi kuishi maeneo hayo hadi mvua zinapowaathiri.

Imekuwa ni kasumba kwa wakazi wa mabondeni kila siku kuhama na kurudi huku wakielewa wazi kwamba maeneo hayo ni hatarishi kwa maisha yao.

Agizo hilo la Mkuu wa Mkoa limekuja wakati muafaka na linatakiwa kuungwa mkono kutokana na athari ambazo zimekuwa zikitokea kila mara kutokana na mvua kwa watu wanaoishi maeneo ya mabondeni.

Kuna kipindi Serikali iliamua kuwatafutia wakazi wa Jangwani maeneo ya Mabwepande ili waondoke katika maeneo hayo. Lakini, kila mwaka mvua zikiisha, watu hao hurudi katika maeneo hayo hatarishi kwa maisha yao na mali zao.

Tunafahamu kwamba kila kipindi cha mvua, watu wengi hupoteza maisha pamoja na mali zao, lakini umekuwa ni utamaduni kila kipindi hicho kikipita watu hurejea tena maeneo hayo.

Pamoja na watu kutambua kwamba maeneo hayo si salama kuishi, bado watu wameziba masikio na kuendelea kuishi katika maeneo hayo.

Inasemekana pia kuna watu walipewa maeneo ya Mabwepande, lakini wameamua kuweka wapangaji katika nyumba zao zilizopo katika maeneo hayo na kuendelea kuchukua fedha za watu, ambao mvua ikinyesha roho zao zipo mikononi mwao.

Hii si mara ya kwanza kwa uongozi wa mkoa huo, kuwaondoa wanaoishi mabondeni. Kila mwaka wamekuwa wakiondolewa na wengine kurejea tena kinyemela. Wengine hawajawahi kuhama Msimbazi, licha ya maafa yanayotokea kila mwaka.

Kuna wengine ambao wameamua kujenga vibanda katika maeneo yaliyobomolewa, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao. Hivyo ubomoaji huo utasaidia kuokoa roho za wenzetu ambao wameamua kwa makusudi kuziweka rehani.

Ni vyema watambue kuna mabadiliko ya tabia nchi ambayo hayatabiriki yatakujaje. Siyo suala la kukaa na kubweteka kuwa wanaweza kumudu mafuriko ya namna yoyote. Waondoe wazo hilo.

Wengi wamekuwa wakiilalamikia serikali baada ya kukumbwa na athari za mvua ile, hali tayari wamepewa maeneo na kurudi katika maeneo hatarishi.

Fedha inayotumiwa na serikali baada ya watu hao kukumbwa na mafuriko ni kubwa, ambayo ingeweza kutumika katika maeneo mengine kuleta maendeleo. Utii wa sheria ni bora, kwa hiyo ni vyema wakaanza kuondoka kuliko kusubiri mpaka serikali ichukue hatua.