Kutenguliwa kauli ya Mwakyembe kusitufanye tubweteke

HIVI karibuni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe aliagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuweka sheria itakayomtaka yeyote anayetaka kuoa au kuolewa, iwe lazima kuwa na cheti cha kuzaliwa kwanza.

Waziri Mwakyembe alisema hadi Mei mwaka huu Rita iwe imehitimisha mchakato huo na kukamilisha sheria. Kwa mujibu wa Mwakyembe, Watanzania wote wanapaswa kujisajili Rita na kuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Hili halina ubishi wala ubaya. Hata hivyo juzi, Rais Dk John Magufuli alitengua kauli ya Waziri Mwakyembe hali iliyoungwa na watu mbalimbali wakiwamo baadhi ya wanasheria pamoja na wananchi mbalimbali.

Pamoja na kuondolewa kwa uamuzi wa Waziri Mwakyembe, wananchi hawapaswi kubweteka, bali kila mmoja ahakikishe napata cheti hicho muhimu na kilicho haki yake.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, ni asilimia 13.7 pekee ya Watanzania ndiyo wenye vyeti hivyo takwimu hizo zinabebwa na Zanzibar inayofikia asilimia 75 ya watu wenye vyeti hivyo.

Kwa mujibu wa Sensa hiyo, Watanzania bado wako nyuma katika kutambua umuhimu wa kuwa na vyeti vya kuzaliwa, jambo ambalo ni hatari kwa siku za usoni.

Kwa mtazamo wangu, changamoto zilizopo katika mchakato wa kupata vyeti hivyo zinapaswa kuwa kichocheo cha kila mmoja kujitokeza kwa kiu zaidi kuvisaka kwani penye nia pana njia.

Ikumbukwe kuwa, umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa ni pamoja na kutumika katika usajili wa huduma mbalimbali ikiwamo elimu kwa mtoto na uthibitisho wa uraia wa mtu.

Kwa msingi huo ndiyo maana ninasisitiza kuwa, kuondolewa kwa agizo la Mwakyembe, hakupaswi kuwafanya watu kulala usingizi au kubweteka na kusahau kutafuta vyeti hivyo.

Ijulikane kuwa, hivi ni kwa manufaa ya mtu na wategemezi wake. Si busara kusubiri kinapohitajika, ndipo mtu aanze kukimbia huku na huko, huku akitoa lawama, wakati nafasi ilikuwapo tena ya kutosha, lakini akaichezea.

Kwa msingi na nafasi hii, ni wakati sasa kila mmoja; wazazi na walezi kuhakikisha watoto na vijana wao wanapata hitaji hili muhimu ambalo huko tuendako, tutafika wakati, mtu akose huduma muhimu kama usajili katika taasisi fulani, kama hana cheti hicho Watanzania wote hatuna budi kuepuka ugonjwa wa kufanya mambo kwa mtindo wa zimamoto sambamba na malalamiko yanayolenga kuficha uzembe wetu na kuusukumiza kwa wengine.

Kuna utaratibu mzuri mama kupewa tangaza anapojifungua na kupaswa kulipeleka Rita ili atengenezewe cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake.

Ninachoamini ni kuwa, wazazi wakitumia utaratibu huu kwa manufaa na Rita wakaboresha huduma za mchakato wa kukipata kwa kuondoa usumbufu unaolalamikiwa sambamba na kuongeza watumishi ili kuondoa kero ya kusubiri cheti kwa muda mrefu.

Hii ni kusema kuwa, Rita ihakikishe inaboresha utaratibu wake ili wananchi wapate huduma hizo na hatimaye, vyeti vya kuzaliwa vipatikane kwa wakati.

Hii ni moja ya mambo yanayowafanya mwananchi wengi kukata tamaa na kusita kufuatilia vyeti vyao wenyewe, au hata vya watoto wao. Rita wakumbuke wanayo dhamana kubwa kuhakikisha Watanzania wengi kama sio wote, wanapata vyeti vya kuzaliwa mapema.