Serikali ya Kenya iwahakikishie usalama madaktari wetu

RAIS John Magufuli amewaruhusu madaktari 500 wa Tanzania ambao hawana ajira serikalini, kwenda kuajiriwa nchini Kenya kama ilivyoomba Serikali ya nchi hiyo.

Hii inamaanisha kwamba Watanzania 500 sasa watakuwa nchini Kenya wakifanya kazi ya udaktari. Hatua hiyo inatokana na Serikali ya Kenya kukiri kwamba ina uhaba mkubwa wa madaktari na hivyo inahitaji waongezwe.

Kama Watanzania lazima tufurahie hatua hiyo, kwamba ndugu zetu wanaenda kupata ajira na hivyo kuongeza na kuboresha uchumi wao na wa taifa letu. Kwamba mishahara watakayoipata itarudi nchini kwa lengo la kuijenga nchi yetu.

Rais Magufuli wakati akizungumza baada ya kutembelewa na ujumbe kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba Kenya ni ndugu zetu, hivyo kama kuna upungufu wa madaktari, Tanzania inawajibika kuwasaidia kama inao wa akiba.

Na kwa maneno yake akasema kwamba Tanzania inayo ziada ya madaktari ambao tangu wamalize masomo yao hawajapata ajira; hivyo akasema ni vyema wakaenda nchi jirani wakapate ajira kwa manufaa yao na taifa.

Mara tu baada ya Rais Magufuli kukubali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jinsia, Wazee na Watoto kupitia katibu wake mkuu ikatoa tangazo la kazi nchini Kenya kwa madaktari ambao hawafanyi kazi katika serikali wanaweza kuomba kazi hiyo.

Chama cha Madaktari (MAT) kupitia kwa kiongozi wake Obadia Nyongole, kimepongeza hatua hiyo, lakini kimeonesha wasiwasi kuwa usalama wa madaktari hao unaweza kuwa hatarini kutokana na msuguano uliopo baina ya Serikali na madaktari.

Licha ya wajumbe wa Rais Kenyatta, kueleza kuwa wameomba madaktari hao kutokana na uhaba uliopo nchini mwao na kwamba hilo lilikuwa moja ya sharti katika mgomo wa madaktari kwamba wako wachache hawatoshi, lakini MAT bado inaonesha kwamba usalama kwa madaktari wetu utakuwa ni mdogo.

Hoja ya MAT imefafanua kuwa endapo madaktari hao watakwenda bila mgogoro wao kwisha, mazingira na utendaji kazi utahatarisha usalama wa madaktari hao.

Niwahamasishe Watanzania wenzangu wenye sifa kuhakikisha wanachangamkia fursa hii adimu kutokea. Kwa kuwa mmesoma kuhudumia watu, hata Wakenya ni watu hivyo nendeni huko mkawasaidie kuokoa maisha ya watu. Lakini angalizo hili la MAT ni la msingi mkubwa.

Kwamba tusije tukafurahia upatikanaji wa ajira hizo, kumbe ndugu zetu wakienda huko wakaanza kuhujumiwa au kuweka usalama wao rehani.

Binafsi nashauri kwamba Serikali ya Kenya licha ya kuwaahidi kuwapa mishahara mizuri na nyumba za kuishi, lakini iongeze kipengele cha kuwapa ulinzi wa uhakika.

Nasema hivyo kwa sababu siamini kwamba madaktari wa Kenya watafurahia kuona kwamba, Watanzania wanaenda kufanya kazi na wao huku wakipata maslahi mazuri yawezekana kuliko hata wanayopata Wakenya.

Ni jukumu sasa la Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba madaktari ambao Tanzania imewapa, wanakuwa salama wao na familia zao. Wanakuwa salama kuanzia wanakoenda kufanya kazi na wanakuwa salama wanapokuwa nyumbani.